Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam Mhe *Janeth Mahawanga* amekuwa Mgeni Rasmi katika hafla mahususi ya WanaVicoba na wasio wanaVicoba Mkoa wa Dar es Salaam iliyoandaliwa na Vicoba Brunch ambapo ameweza kuzindua kipindi kipya cha “VICOBA TALK SHOW.”
Hafla hiyo imeweza kuhudhuriwa na vikundi mbalimbali vya Vicoba vinavyopatikana ndani na nje ya ya Mkoa wa Dar es Salaam sambamba na Taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya kuwainua Wanawake kiuchumi, Wadau wa maendeleo, Wataalam wa masuala ya Uchumi na fedha, Fursa, Saikolojia, Uwekezaji, Masuala ya Bima kwa Vikundi na Wataalam wa Teknolojia na Masoko.
Pia amezindua kipindi cha Vicoba Talk Show kwa ajili ya wanawake wanaojihusisha na Vicoba kitakachoweza kutumika kama jukwaa la kujadili changamoto, Kushirikisha wadau wote wa maendeleo kwenye midahalo na mada mbalimbali zinazolenga kuwashika mkono Wanawake Wajasiriamali ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika Hafla hiyo Mh Mahawanga amewepongeza Vicoba Brunch kwa kuweza kukutanisha wanawake kutoka maeneo tofauti jambo ambalo lina tija katika safari ya kumkwamua Mwanamke kiuchumi lakini kuhakikisha Wanawake wanapata mafunzo na kujenga mahusiano mapya na vikundi tofauti vyenye uzoefu na vilivyofanikiwa ili kuwa na utamaduni wa kushikana mikono kwenye safari ya mafanikio bila kuwaacha wengine nyuma.
Aidha Mh. Mahawanga amepongeza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza dhamira yake ya kuwakomboa Wanawake wa Tanzania kiuchumi kupita mikopo isiyo na riba ya asilimia 4% kutoka kwenye kila Halmashauri kwani kupitia mikopo hiyo Wanawake wengi wameweza kunufaika nayo nakwa kiasi kikubwa wameweza kutengeneza ajira miongoni mwao.
Mh. Mahawanga amewasisitiza wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam kuendelea kudumisha upendo, amani, umoja na mshikamano ndani ya vikundi vyao sambamba na kuheshimiana ili waweze kupata mafanikio makubwa zaidi kwani malengo ya Wanavicoba sasa hivi ni kumiliki uchumi wa viwanda vya Wanawake ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Mh. Mahawanga ameshukuru kwa namna ambavyo Wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam wamembatiza jina jipya na kumuita MAMA VICOBA amesema anastahiki kabisa kuitwa hivyo sababu ana uzoefu mkubwa sana na Vicoba kutokana nafasi mbalimbali za Uongozi alizoshika kwenye Vikundi mbalimbali vya Wanawake vyenye mafanikio makubwa na hata hivyo mpaka sasa yeye ni Mwenyekiti wa Kicoba kilichojinyakulia tuzo ya Kicoba bora cha mwaka 2021 Tanzania cha Women of Hope Alive ambacho kinaumri wa miaka kumi sasa na kinafanya vizuri sana.
Pia Mh Mahawanga amewasisitiza sana Wanawake wa Dar es Salaam kupitia vikundi vyao vya Vicoba kuhakikisha wanazitumia ipasavyo fursa zilizopo ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam kwani wao kuwa wana Dar es Salaam ni fursa namba moja hivyo amewaambia wasijichukulie poa wao wamezungukwa na fursa nyingi sana kwani jiji la Dar es Salaam ni jiji la kibiashara na ndio Mkoa uliobeba sura ya Tanzania.