Wanakikundi cha Kididimo Upendo Group wakipata maelezo kuhusu Chimbuko la Mwanadamu kutoka kwa Mhifadhi wa Akiolojia, Bibi Magreth Kigadye walipotembelea Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni
Bibi Prisca Mtakwa, Mtunza Hazina wa Kikundi cha Kididimo Upendo Group kushoto na Bibi Grace Mwigune kulia wakicheza ngoma ya asili Kijiiji cha MakumbushoBi Tabu Kimote aneonesha mfano wa kusaga kwa kutumia jiwe maalun pamoja na Bi Linda Makoye ambaye anatumia mchi na kinu kutwangwa baada ya kupewa maelezo kuhusu vifaa walivyokuwa wanatumia wangoni wa kwaajilia ya kuandaa chakula kwa mfano utengeneza unga na nafaka zingine.
………………..
Na Mwandishi Wetu,
Kikundi cha Wastaafu kutoka kijiji cha Kididumo, Mkoani Morogoro wametembelea Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni pamoja na Kijiji cha Makumbusho na kuwataka wastaafu kutumia muda wao vizuri kwa kutembelea vivutio mbalimbali nchini.
Mlezi wa Kikundi hicho cha Kididimo Upendo Women Group and Familiy, Dkt. Peter Mtakwa amesema kuwa wastaafu wanaweza kutumia muda walionao kufanya utalii wa ndani ikiwa ni pamoja na kutembelea vituo vya makumbusho ya Taifa ambapo wanaweza kujifunza vitu vingi.
“Natoa wito kwa wastaafu wenzangu kutumia fursa ya muda walionao na rasilimali walizonazo kufanya utalii wa ndani kwa lengo la kuburudika na kujifunza wasingoje mpaka waishiwe nguvu kabisa, amesema Dkt Mtakwa ambaye alikuwa mwalimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine.
Amesema kuwa katika jiji la Dar es Salaam kumekuwa na mabadiliko makubwa na vitu vingi vipya ambavyo havikuwepo miaka ya nyuma ambavyo wananchi wangeweza kuviona na kujifunza ikiwemo, daraja la Kigamboni, Daraja la Tanzanite, majengo, maoneshoo mapya Makumbusho ya Taifa na vingine vingi.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Bibi Dyness Kilonzo amesema kuwa wamekuwa wakitembelea maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufanya utalii lakini hawakuwahi kutembelea Makumbusho na kwamba walikuwa hawajui kuwa kuna vitu vingi vya kujifunza.
“Wajukuu wamekuwa wakituuliza maswali kuhusiana na historia ya Tanzania na vitu mbalimbali vinavyopatikana Makumbusho hatukuwa na majibu sahihi lakini sasa tunayo majibu ya kuwaambia wajukuu zetu,” amesema Bibi Kilonzo.
Amesema wamefurahishwa sana na vitu vingi vinavyopatikana Makumbusho ya Taifa na kuahidi kutoa elimu kwa wengine kutembelea Makumbusho za Taifa ambapo watajifunza vitu vingi.
Wajumbe wengine wamesema safari yao ilikuwa nzuri na wameona vitu vingi ambavyo walikuwa wanatamani kuviona.
Naye Afisa Uhusiano Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Bi Joyce Mkinga aliwakaribisha wastaafu hao wapatao 30 na kuwaomba kuendelea kutoa elimu kwa wastaafu wengine kutembelea vituo vya makumbusho na malikale ambavyo viko maeneo mbalimbali ya Tanzania.
“Tumefurahia ujio wenu kama senior citizen karibuni sana Makumbusho ya Taifa nasi tupo tayari kuwahudumia,” alisema Bi Mkinga.