Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri Omary Kumbilamoto (katikati),Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Dar es salaam Tabu Shaibu (kushoto) na Kaimu Meya wa Halmashauri ya jiji la Dar es salaam (kulia).Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilala Mhandisi Silvesta Chinengo akitolea ufafanuzi baadhi ya changamoto za miundombinu ya barabara katika kata za jiji hilo.Madiwani wa Halmashauri ya jiji la Dar es salaam walioshiriki katika kikao cha robo ya nne cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya jiji hilo.
…………………….
NA MUSSA KHALID
Madiwani wa Halmashauri ya jiji la Dar es salaam wameiomba wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini –TARURA kutekeleza kwa wakati uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika jiji hilo ili kuondoa adha kwa wananchi.
Hayo yamejiri leo jijini Dar es salaam katika kikao cha robo ya nne cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya jiji hilo ambapo baadhi ya madiwani wameitaka TARURA kuboresha miundombinu hiyo kutokana na kuepo kwa changamoto hasa ya usafirishaji na watu kupita.
Akizungumza katika Kikao hicho Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es salaam na Mwenyekiti wa Baraza hilo Omary Kumbilamoto amesema katika Bajeti ya mwaka wa fedha wametenga Takriban Bill 6.2 hivyo ameahidi kuwa watampa ushirikiano Meneja TARURA ili utekelezaji huo ufanyike kwa haraka.
‘Moja katika taarifa ambazo tumeweza kuzijadili ni suala la miundombinu ya barabara na tumshukuru sana Rais wetu Mpendwa Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwa zile halmashauri ambazo zinakusanya fedha nyingi basi zitenge fedha zake kwa ajili ya barabara hivyo sisi tumetenga Takriban Bill 6.2’amesema Meya Kumbilamoto
Aidha Mstahiki Meya Kumbilamoto amesema kuwa kwa sasa mifumo ya fedha imekwishafunguka hivyo wanatarajia kuanza utekelezaji wa miradi ya barabara kwa haraka.
Kwa upande wao baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wameisisitiza TARURA kudhibiti mashimo korofi katika barabara zilizopo katika kata zao.
Wamesema kuwa ni vyema TARURA ikatekeleza ujenzi wa miradi hiyo kwa wakati kwani itasaidia kurahisisha huduma mbalimbali za jiji kutokana na kutumika katika usafirishaji.
Akijibu malalamiko kutoka kwa madiwani hao Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilala MhandisiSilvesta Chinengo amesema kuwa wamekuwa wakikumbana na changamoto katika utekelezaji wa miundombinu ikiwemo ufinyu wa bajeti lakini pia uharibifu wa miundombinu.
Pia amesema amewaahidi madiwani kuwa watahakikisha wanakaa na wataalamu wa Jiji ili waweze kuandaa mpango kazi watakao kubaliana kwa ajili ya utekelezaji.