Diwani wa Kata ya Minazi Mirefu jimbo la Segerea Halmashauri ya jiji la Dar es salaam Godlisten Malisa.
moja ya Kamera ya Kisasa (picha na mtandao)
………………
NA MUSSA KHALID
Kata ya Minazi Mirefu jimbo la Segerea Halmashauri ya jiji la Dar es salaam imejipanga kufunga Kamera za kisasa katika barabara zote kubwa zinazozunguka kata hiyo ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi wake.
Akizungumza na Kituo hiki jijini Dar es salaam Diwani wa Kata hiyo Godlisten Malisa amesema lengo la ufungaji wa Kamera hizo pia ni kulirahisishia Jeshi la Polisi kufanikisha kwa urahisi udhibiti wa matukio mbalimbali yanayofanywa na wahalifu.
Diwani Malisa amesema kuwa mipango yao ni kuhakikisha wanafunga Kamera hizo katika maeneo ya makutano,vituo vya waendesha bodaboda na bajaji pamoja na maeneo yaliyorahisi kupitika kwa watu wenye nia ovu.
Aidha kuhusu zoezi la ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Minazi Mirefu Diwani Malisa amesema wanatarajia kuanza ujenzi mwezi wa 11 mwaka huu kwani lengo ni kusaidia kuimarisha masuala ya ulinzi kwa ukaribu na siyo kwenda mbali mpaka Buguruni.
‘Kuanzia Mwezi huo wa 11 tutaanza ujenzi na katika ushirikiano na Polisi wanatupa ushirikiano sababu ndio wametupa ramani nzima hivyo suala la kwenda buguruni litakuwa limefutika kwani huduma zote zitapatikana katika kata yetu’amesema Diwani Malisa
Hata hivyo wananchi wa Kata hiyo wametakiwa kuendelea kuwaonyesha ushirikiano wa karibu kwa serikali ya Kata hiyo ili iweze kufanikisha kwa wakati miradi mbalimbali ya kimkakati iliyoipanga kuitekeleza.