Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, amesema Chama kinaridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa daraja la JP Magufuli linalounganisha kati ya Mkoa wa Mwanza na Geita ambalo linajengwa eneo la Kigogo-Busisi.
Akizungumza wakati akikagua daraja hilo Kinana ambaye yupo katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, amesisitiza daraja hilo ujenzi wake unakwenda kwa wakati kama ilivyopangwa, hivyo mwaka 2024 nchi itakuwa imepata alama kubwa ya kuwa na daraja refu lenye urefu wa karibu kilomita 3.2.
“Najaribu kukumbuka madaraja mangapi katika Afrika yenye urefu huo kama hili halitwakua la kwanza basi litakuwa katika tatu bora. Hivyo niwapongeze wote wanaoshiriki ujenzi wa daraja hili ndugu zetu wa kutoka Korea, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajenzi kutoka Kampuni ya China na Watanzania wote wanaoshiriki,” amesema Kinana.
Kinana akiwa kwenye daraja hilo baada ya kulikagua na kupata maelezo ya ujenzi wake ambao umefikia asilimia 51, amepata nafasi ya kuwasilimia wajenzi wa daraja hilo na kuwapongeza kwa kazi nzuri.
“Mnafanya kazi nzuri sana, mnafanya kazi kubwa na Rais (Samia Suluhu Hassan) ametumina nije niwasalimie na niwambie kwamba anangojea aje kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa daraja hili litakapokamilika,” amesema Kinana.
Awali Mhandishi Mshauri wa ujenzi wa daraja hilo Abulkarika Majuto ameelezea hatua kwa hatua kuhusu ujenzi huo ambapo amesema kwa sasaa umefikia asilimia 51.
“Tunakukaribisha kwenye ujenzi wa daraja la JP Magufuli ambalo lina urefu wa kilomita 3.2 pamoja na barabara unganishi za kilomita 1.66 na kwamba daraja hili litakapokamilika litaziunganisha wilaya mbili za Sengerema na Misungwi ambazo zinatenganishwa na Ziwa Victoria kwa kupitia barabara ya kupitia Usagara, Sengerema hadi Geita.
“Barabara hii ya Usagara, Sengerema hadi Geita ni miongoni mwa barabara ambazo zinapita katika ukanda huu wa Ziwa Victoria na utekelezaji wake ni miaka minne ambapo unatarajia kukamilika Februari 24, mwaka 2024.
=========