MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, amelakiwa na viongozi wa Chama na Serikali Mkoa wa Mwanza baada ya kuwasili mkoani hapa akitokea Mkoa wa Geita kwa ziara ya kikazi.
Kinana amewasili Mwanza leo Septemba 4, 2022 na kupokelewa katika Kijiji cha Igaka, Kata ya Buzilasonga wilayani Sengerema mkoani Mwanza. Miongoni mwa viongozi waliomlaki ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa Athony Dialo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima.
Ziara za Kinana zinalenga kukagua uhai wa Chama hicho pamoja na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020/2025.
Pamoja na mambo mengine, Kinana baada ya kuwasili wilayani Sengerema amezindua ofisi ya CCM ya wilaya hiyo ambapo ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wana CCM kwa ujenzi wa ofisi hiyo.
Pia, amekagua ujenzi wa daraja la JPM ambalo linajengwa katika eneo la Kigogo-Busisi linalounganisha Mkoa wa Mwanza na Geita.
Kinana aliyeambatana na Katibu wa Halashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akiwa Mwanza atakutana na wana CCM na kufanya mikutano ya ndani pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.