……………………..
Wizara ya Maliasili na Utalii leo Septemba 04, 2022 jijini Dodoma imewasilisha mada kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo kuhusu marekebisho ya Sheria ya Mambo ya Kale Sura 333 na Sheria ya Makumbusho ya Taifa Sura 281 ili kutoa fursa kwa Wajumbe wa kamati hiyo kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu marekebisho ya sheria hizo.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa semina hiyo Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Mhe Balozi Dkt Pindi Chana, amesema pamoja na semina hiyo kujikita katika marekebisho ya Sheria ya Mambo ya Kale pamoja na sheria ya Makumbusho pia inatoa fursa kwa wajumbe wa Kamati kujadili na kutoa mapendekezo namna bora ya kuzifanyia marekebisho sheria hizo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo, Mhe. Kilumbe Shabani Ng’enda (Mb) pamoja na wajumbe wengine wa kamati hiyo wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kujipanga vyema katika kufafanua marekebisho ya sheria hizo na wao kama Kamati wataendelea kushirikiana na Wizara ili kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na Malikale zilizopo.