Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMA) Dkt Agnes Kijazi akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka huu ambapo amesema kutakuwa na upungufu wa mvua wakati mamlaka hiyo ilipotangaza utabiri Makao Makuu ya TMA Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Septemba 02.2022.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMA) Dkt Agnes Kijazi akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka huu ambapo amesema kutakuwa na upungufu wa mvua.
Mtabiri wa hali ya hewa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA Bi. Rosemary Senyagwa akiwasilisha utabiri wa mvua za Vuli wakati mamlaka hiyo ilipotangaza utabiri huo leo Makao Makuu ya TMA Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Sepatemba 02.2022.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania -TMA imesema katika kipindi cha mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza Mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka huu kutakuwa na vipindi virefu vya ukavu na kuna uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ambayo inaweza kuleta athari.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMA) Dkt Agnes Kijazi ameeleza hayo leo jijini Dar es salaam wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka huu ambapo amesema kutakuwa na upungufu wa mvua katika kipindi hicho hali itakayosababisha kupungua kwa unyevunyevu katika udongo hivyo kuleta athari mbalimbali.
Dkt Kijazi amesema kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na inavyotarajiwa katika kipindi chote cha msimu kwa ujumla mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
‘Maeneo ya Kanda ya Ziwa Viktoria: (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kibondo na Kakonko)): Mvua zinatarajiwa kuwa za Chini ya Wastani hadi Wastani katika maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa Victoria. Mvua hizi zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2022 katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (Wilaya za Kibondo na Kakonko). Aidha, katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Simiyu mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2022. Mvua zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2023’amesema Dkt Kijazi
Kuhusu athari zinazoweza kujitokeza katika sekta ya kilimo Dkt Kijazi amesema kuwepo kwa ongezeko la visumbufu vya mazao kama vile mchwa, viwavijeshi, nzige na panya hivyo amewashauti wakulima kupanda kwa wakati na kutumia mbegu na mazao yanayoweza kukomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili ukame.
Amewataka wakulima kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa ugani juu ya kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo na uvunaji wa maji ya mvua.
Awali akieleza tathmini ya mvua za masika msimu uliopita pamoja na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa kwa mfumo wa mwaka 2022 ,Mtaalamu wa Hali ya Hewa TMA Rose Senyagwa amesema kuwa kiwango cha usahihi wa utabiri kilikuwa ni asilimia 95.7 ikiwa ni ongezeko la 5.2% ukilinganisha na msimu uliopita.
Hata hivyo Mamalaka hiyo imezishauri Menejimenti Za Maafa kushirikiana na kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula,
malisho ya mifugo, maji na kutoa miongozo ya namna ya kukabiliana na maafa ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza