Wasichana wanaowezesha programu ya stadi za maisha “Dunia Yangu Bora” ya Shirika la CAMFED, kwa mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika moja ya kikao kazi. |
JUMLA ya Wanafunzi 70,302 kutoka katika shule za sekondari mbalimbali nchini Tanzania wananufaika na progamu ya Dunia Yangu Bora inayofundisha stadi za maisha kwa wanafunzi hasa wa kidato cha kwanza na chapili, programu inayoratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali la CAMFED Tanzania.
Takwimu hizo zimetolewa juzi jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Wanafunzi wanaotoa elimu hiyo shuleni kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Asha Kassim alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi cha viongozi wa wanafunzi watoa elimu kupitia progamu ya Dunia Yangu Bora.
Alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam jumla ya shule za Sekondari 64 zipo katika mpango huo wa elimu zikitoka katika Wilaya za Ilala, Temeke, Kigamboni, Kinondoni pamoja na Wilaya ya Ubungo.
Akifafanua zaidi alisema kwa Tanzania nzima takribani shule 493 ambazo zinatoka katika mikoa 10 nchini, zinanufaika na elimu hiyo, huku zikiwa na wanafunzi wa kike 37,925 na wanafunzi wa kiume 32,377.
Aliongeza kuwa nia na madhumuni ya mradi huo ni kuwasaidia wanafunzi walioko shuleni hasa kidato cha kwanza na cha pili kujisaidia kujitambua, kujijua wao ni nani na wanatakiwa kufanya nini, ili kuweza kufikia malengo yao waliojiwekea.
“….mpango huu pia unasaidia wanafunzi hao kuweza kumaliza masomo yao, kuwafuatilia wanafunzi walioacha shule kuwashauri na kuwatia moyo ili warejee shuleni na kuendelea na masomo yao, wawezeshaji wa wanafunzi katika mradi huo hawaishii shuleni pekee lakini hata kuwasaidia kiushauri na mwongozo wasichana wanaopata changamoto mbalimbali katika jamii.”
“…Sisi kama wawezeshaji huwa tunawatembelea watoro majumbani na kuzungumza nao nini changamoto zao, taarifa za watoro huwa mara nyingine tunapewa na walimu au wanafunzi shuleni na kuanza kuwafuatilia, mara nyingine huwa tunaipata kupitia programu zetu tunazoziendesha shuleni,” alisema.
Alisema wapo wanafunzi watoro ambao wanapowatembelea majumbani na kuzungumza nao kirafiki huweka wazi sababu ya wao kutokuja shule, ambapo ni kuchangiwa na changamoto za kifamilia na tunapofanikiwa kuzitatua mwanafunzi huwa anarudi shuleni na kuendelea na shule kama wenzake.
“Kuna vijana wengine huamua tu kukataa shule labda hajui umuhimu wake na uhusiano wake na maisha yake ya baadaye…vijana kama hawa sisi hukaa nao na tunawapa elimu ya umuhimu wa shule na kuwashauri vizuri na kujikuta wakirejea shuleni,” alisema Bi. Asha Kassim akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Kwa upande wao, miongoni mwa wanafunzi viongozi ambao hutoa elimu hiyo shuleni, Experansia Yosia (Mizimbinu Sekondari), Sara Jeseph (Kinyerezi Sekondari) na Moza Athumani (Buza Sekondari) walisema mbali na kutoa elimu ya stadi za maisha na kujitambua kwenye shule walizopangiwa pia husaidia jamii mitaani kwao wanapopatwa na changamoto za unyanyaswaji kutoka kwenye familia zao.