Kaimu kamanda wa polisi kanda maalum Dar es salam ACP William Mkonda
……………………
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linaendelea na operasheni kali ya kuzuia vitendo vya kihalifu ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahalifu waliotenda makosa ya kijinai ya siku za nyuma katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.
Katika hatua hiyo Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa 15 kwa tuhuma za uvunjaji na kuiba vifaa mbalimbali vya ujenzi katika Ghala la VOILA Trading CO (T) LTd linalomilikiwa na raiwa wa China.
Jeshi la Polisi lilipokea taarifa juu ya watuhumiwa hao kuvunja na kuiba vifaa hivyo ndani ya Ghala hilo lililopo eneo la Kiwalani Wilaya ya Ilala Dar es Salaam ambapo Jeshi la Polisi lilifanya upelelezi na ufuatiliaji wakina na tarehe 27/08/2022 majira ya 7:00 usiku lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa na mali za wizi zikiwemo maboksi 17 ya Angles, door closer maboksi 6, lock maboksi 4, Project handle maboksi mawili, cutting disc maboksi 9, Slider boksi 1, maboksi ya Chandarua mabegi 37 na arms boksi 1 pamoja na gari lenye namba za usajili T 478 DXU aina ya Toyota Hino.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamtafuta mtuhumiwa wa wizi wa basi la Daladala lenye namba za usajili No. T 812 DCL Toyota Coaster ambalo tarehe 23/08/2022 liliripotiwa kuibiwa maeneo ya Chanika Ilala Dar es Salaam.
Baada ya taarifa hizo Jeshi la Polisi liliendelea na ufuatiliaji ambapo tarehe 25/08/2022 lilifanikiwa kulipata basi hilo limeegeshwa maeneo ya Tabata Chang’ombe likiwa halina baadhi ya vifaa vya injini ambavyo thamani yake bado haijafahamika.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam linaendelea kumtafuta mtuhumiwa mwingine wa wizi wa basi lenye namba za usajili T. 505 DTW aina ya Mitsubishi Rosa lililoibiwa tarehe 27/08/2022 maeneo ya Gongolamboto Ilala Dar es Salaam ambako katika upelelezi ilionekana linasafirishwa kwenda nje ya jiji.
Amesema katika ufuatiliaji zaidi majira ya 04:00 asubuhi gari hilo lilikutwa maeneo ya Kibaha Loliondo limetelekezwa na mtuhumiwa ambaye alikimbia baada ya raia wema kumtilia shaka na kupigiwa kelele za mwizi.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam linaendelea na msako mkali wa kuwakamata wahalifu wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu na malengo ni kuhakikisha watu wanafanya shughuli zao katika mazingira yaliyo salama, bila hofu na kwa kuzingatia sheria za nchi.
WILLIAM MKONDA – ACP
KAIMU KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAM.