***********************
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana leo Agosti 27, 2022 ameendesha Kikao kazi cha Wakuu wa Vyuo vya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kupokea taarifa za uendeshaji wa vyuo hivyo.
Akizungumza na Wakuu wa Vyuo hivyo Waziri Balozi Dkt.Pindi Chana amesema Wizara anayoiongoza imedhamiria kuweka mfumo wa usimamizi wa vyuo hivyo pamoja na kuendelea kufanya maboresho ya miundombinu na mazingira ya kufundishia ili viendelee kutoa elimu bora kwa Watanzania
“Ni dhahiri mabadiliko haya yatahitaji kuendana na utoaji wa elimu ya Uhifadhi na Utalii ili kuzalisha wataalam wenye uwezo wa kusimamia vyema sekta Sekta ya Wanyamapori, Misitu na Nyuki ambazo zimekua na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi” . Alisisitiza Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
Licha ya kuwapongeza viongozi wa vyuo hivyo kwa kazi nzuri wanayofanya ya kutoa elimu kwa Watanzania, Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameeleza kuwa juhudi zaidi zinahitajika ili kuhakikisha malengo ya vyuo hivyo kwa Wizara yanafikiwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka ameziagiza Taasisi hizo za Elimu kutumia changamoto zilizopo kama fursa kwa kuvifanya vyuo hivyo kuendelea kujenga uwezo kwa kutumia mazingira, rasilimali na nguvu kazi wanayozalisha kubuni miradi na kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato.
Wizara ya Maliasili inasimamia na kuendesha vyuo vya Taaluma vya Usimamizi wa Taaluma ya Wanyamapori, Misitu na Nyuki ambavyo ni Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA), Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori -Pasiansi, Taasisi ya Mafunzo ya Ufugaji Nyuki – Tabora, Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi kwa Jamii – Likuyu Sekamaganga, Taasisi ya Mafunzo ya Misitu Olomotonyi (FTI) na Taasisi ya Viwanda vya Misitu ( FITI).