MAMLAKA ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Morogoro, imewafikisha mahakamani watuhumiwa sita kwa makosa matatu likiwemo la kushindwa kuomba kusajiliwa kwenye kodi ya ongezeko la thamani VAT.
Washitaki hao walifikishwa mahakama ya wilaya ya Kilosa tarehe 25 mwezi wa nane 2022 na kusomewa mashitaka na Mwendesha mashitaka mwandamizi wa Serikali Cherubini Chuwa mbele ya hakimu mkazi mfawidhi Agnes Ringo .
Washitakiwa hao ni Kibwana Kidinilo, Kitete Sugar, Clement Gwila na Mathias Mligwa ambao walifika mahakamani huku Gajoki LTD na Green Line Brothers hawakufika mahakamani hapo na hivyo mahakama iliagiza watafutwe na kufikisha mahakamani.
Akisoma mashitaka hayo mwendesha mashitaka Chuwa alisema washitakiwa hao walitenda kosa hilo Julai 26 mwaka huu, kwa nyakati tofauti wakati.
Alisema makosa wanayokabiliwa nayo ni kushindwa kuomba kusajiliwa kwenye kodi ya ongezeko la thamani VAT, kinyume kifungu 28 cha sheria ya kodi ya VAT sura 148, ikisomwa pamoja na kifungu Cha 90 (1) cha sheria ya usimamuzi wa kodi namba 10 ya mwaka 2015 yenye marejeo hadi mwaka 2019.
Alitaja kosa la pili ni kuwazuia maafisa wa TRA kufanya kazi yao kwa kukataa kwa makusudi kurejesha fomu za VAT walizopewa, kinyume na kifungu cha 85 (3) (I) cha sheria ya usimamuzi wa kodi namba 10.
Alisema shitaka la tatu wanalokabiliwa nalo ni kushindwa kuendana na matakwa ya sheria za kodi kwa kutofika kwa hiari kusajiliwa na VAT.
Hata hivyo washitakiwa wote walikana mashitaka huku wakuachiwa kwa dhamana ya wathamini wawili wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya sh milioni ishirini kila mmoja ambapo kesi hiyo itatajwa tena Agosi 31 mwaka huu.