WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza na Mwandishi wa BBC Salim Kikeke Katika mahojiano naalum kuhusu sheria ya Habari.
Neville Meena Mjumbe wa Kamati Tendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF.
………………………………….
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema, waandishi wa habari wasimamie mambo yao wenyewe.
Waziri Nape ametoa kauli hiyo tarehe 24 Agosti 2022, wakati akizungumza katika kipindi cha BBC Swahili – Dira ya Dunia, jijini Dar es Salaam.
“Waandishi wa habari kama wanataaluma zingine, wajisimamie wenyewe na inawezekana. Sisi kama serikali tubaki na vitu vichache sana vinavyolinda nchi, usalama na afya ya jamii, lakini mengine mengi yafanywe na wanahabari wenyewe.
“…na inawezekana maana madaktari wamefanya imewezekana, wanasheria wamefanya imewezekana na wanahabari inawezekana,” amesema Nape.
Akizungumzia Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 inayompa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo mamlaka makubwa, amesema sheria hiyo ililenga kupunguza madaraka aliyopewa mkurugenzi huyo katika Sheria ya Habari ya Mwaka 1976.
Sheria hiyo inampa mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kufungia vyombo vya habari, kutoa leseni na hata kufuta eleseni ya mwanahabari jambo ambalo linalalamikiwa na wadau wa habari nchini.
“Duniani kote ukitaka haki itendeke, ni muhimu anayelalamika, anayetengeneza mashitaka na anayekwenda kusikiliza mashitaka wawe ni watu tofauti ili haki itendeke.
“Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo tunataka madaraka yake yapunguzwe,” amesema Nape akisisitiza Sheria ya Mwaka 2016 imepunguza zaidi mamlaka ya mkurugenzi huyo ikilinganishwa na ile yam waka 1976.
Nape alisema, sio jambo rahisi kwa mlalamikaji kusimamia na kutoa kesi katika kesi anayoilalamikia mwenyewe, na kwamba sasa wanataka madaraka ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo yapunguzwe.