…….,……………
eladius Makwega-Mlali, Kongwa DODOMAKwa hakika nilifika katika Mji wa Lushoto na kupokelewa vizuri na shemeji zangu Wasambaa, ndugu zangu hawa wakiwa ni watu wazuri ukizungumza nao jambo mnakubaliana vizuri sana, labda changamoto inakuja katika utekelezaji tu wa jambo hilo.
Kwa hakika nilifanya kazi kwa moyo wangu wote nikiamini kuwa hapa hata kama nitatumbulia lazima nitarudi katika mji huu kwa hoja ya kuwa hapa ni ukweni na wanangu ni ujombani. Japokuwa urithi wa ujombani kwa wanangu ni tonge tu.
Kazi nilianza kufanya vizuri huku nikipokelewa na Mwenyekiti wa Halmashauri hii mheshemiwa Lukas Shemndolwa, diwani mmoja mtulivu, mwelewa akiwa na uzoefu wa udiwani na Uenyekiti kwa miaka mingi.
Nilifanya kazi hii kwa miezi kama sita hivi huku nikijitahidi kupambana na changamoto za hapa na pale, kanuni ikiwa hakuna kulalamika iwe kwa mdomo au maandishi ni kukabiliana nazo tu.
Wakati huo mkuu wa mkoa wa Tanga alikuwa ni ndugu yangu Martine Shigella( sasa yu Geita) yeye alikuwa na uzoefu mkubwa wa masuala haya tangu akiwa Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa na aliwahi kuwa mkuu wa wilaya na hata mshauri wa rais wa masuala ya kisiasa.
Shigella ni mtu mtulivu sana, msikivu sana, mfuatiliaji sana wa mambo, hapendi uonevu kwa yoyote yule, huku hapendi waliochini yake mambo yaharibike akiwa yeye ni msimamizi/kiongozi.“
Jamani mkiwa na jambo gumu mtujulishe, siyo mnakaa kimya hadi Rais anauliza alafu miye sifahamu, hilo siyo jambo zuri, akiuliza haya Shigella Lushoto kuna nini? Niwe ninafahamu mapema, sawa jamani?”
“Sawa mkuu.” Tulijibu sote tulioshiriki kikao hicho kilichofanyika Tanga na kilipomalizika tulirudi katika halmashauri tulizokuwa tunafanyia kazi.
Nilipofika Lushoto jioni hiyo nikalala na asubuhi nikaamka kujianda ili kuelekea ofisini, nyumba ya mkurugenzi mtendaji wa wilaya eneo ilipo ni njia panda ambapo ni vigumu kwa mgeni wa mji huo kujua kama hapo kuna makazi.
Siku hiyo ilikuwa na mvua kubwa ikinyesha kwa hiyo gali lilifika kwa tabu kwa kuwa kulikuwa na tope jingi njiani, hata lilipofanikiwa kufika kwa mbinde dereva aliyefahamika kama John Kyando(Mhehe–Mbondei) alishuka na kuamua kuchukua mpira wa maji ili kupunguza tope kwenye matairi ya gali hilo.
Akauvuta mpira vizuri , ikabidi aende kufungua bomba hilo ili litoe maji aanze kupunguza tope, akapanda kama ngazi kuelekea katika bomba hilo, kushoto kwake kukiwa na shina la mgomba wa jamaika unaozaa sana na kwa mbele yake kukiwa na banda la kuku na mbuzi.
Wakati anataka kufungua maji, akiwa jirani na banda la wanyama hao akaona wanyama hao wamelala chini, ah kulikoni? Kuku, khanga, bata na mbuzi. Alipochungulia vizuri akabaini kuwa mifugo hiyo kama ilichinjwa katika nyumba ambayo inajiandaa na sherehe.
Alipoingia bandani alibaini kuwa kweli walichinjwa na hata alipozunguka nyuma ya banda alibaini kuwa mbwa na yeye kisu kilimtembelea kooni mwake.“Hapa kuna shida, si bure.” Alisema dereva huyo mshika dini.
Akawajulisha wale walikuwapo jirani naye, nikajulisha juu ya tukio hilo, huku mimi nikijulisha kituo cha polisi jirani tukio hilo. Uchunguzi ukawa unaendelea, miye nikaelekea kazini.
Ushauri ukatolewa kuwa walinzi ambao walikuwa mgambo wanaolinda makazi hayo wabadilishwe na wakaletwa mgambo wengine ambao walikuwa na mchanganyiko maalumu kutoka malindo mengine.
Polisi wakaendelea na uchunguzi, huku sasa kukiwa na ulinzi mzuri nalo Jeshi la Polisi la wilaya ya Lushoto wakati huo likiwa jirani likiongozwa na OCD Maziwa(marehemu kwa sasa) na OSS Georgina Matagi kwa karibu mno wakiongeza nguvu katika makazi hayo.
Siku iliyofuata maisha yaliendelea kama kawaida naye dereva Kyando alifika nyumbani hapo na kunichukua hadi ofisini, tulipofika jirani na jengo la halmashauri ya wilaya nikashangaa watu wapo nje hawajaingia ofisini, kwenye mlango mkuu, huku tukijiuliza leo halmashauri kuna nini mbona watumishi wapo nje? Tulijiuliza mimi na dereva, hatukupata majibu. Niliposhuka watumishi wakakaa kando hili kunipisha njia.
Mimi nikapanda ngazi kadhaa nakutaka kuingia ndani ya mlango mkuu wa halmashauri nikaambiwa,“Mkurugenzi usivuke, mkurugenzi usivuke, mkurugenzi usivuke, mkurugenzi usivuke.”Hapo gafla nikakimbiliwa na watumishi wawili wa ofisi ya mkurugenzi mtendaji mmoja anaitwa Fatuma na mwingine anaitwa Beatrice wakiwa wameshika mifagio wakaniambia,“Tulipofika hapa tumekuta damu zimemwaga, kama hivi unavyoziona, sasa kila mmoja anaogopa kufanya usafi na hata kuingia ofisini na sisi ndiyo tunataka kuzifuta muda huu, kwa hiyo ngoja kwanza tuzifute.”
Fatuma na Beatrice ambao hilo halikuwa jukumu lao, lakini walifanya hivyo na mimi nikaungana nao kufanya usafi na kuwatia moyo watumishi wengine, hapo ndiyo wakapata moyo wa kujiamini na kunipokea fagio , nikafunguliwa mlango dharura na mimi kuingia ofisini na watumishi wengine kuingia katika jengo hilo ili kazi zianze kufanyika baada ya lango kuu kufunguliwa.Jambo hilo likileta taharuki kubwa ofisini hapo.
Watu wa kwanza kuulizwa walikuwa ni walinzi wa zamu ya siku hiyo,“Sisi hatufahamu lolote, labda hapo itaNyuma ya pazia kukiwa na simulizi iliyokuwa ikienea kuwa,“Huyu mkurugenzi anatoka pwani, unapotaka kuwalogwa waswahili unatumia vitu vyao mwenyewe, hasa hasa wanyama wanaufugwa nyumbani kwake.
Kwa hiyo mifugo yake ilichinjwa na kwenda kufanyia ushirikina na huo ushirikina kumwaga katika mlango wa ofisi ya jengo kuu la halmashauri.”Sasa akilini kwangu nikakumbuka yale maelezo ya Martine Shigella alivyosema,“Mkiwa na jambo mtujulishe mapema, siyo mnakaa kimya, hata Rais akiuliza, haya Lushoto kuna nini , wewe hujasema, semeni mapema jamani.
”Je utamsimulia vipi mkuu wa mkoa juu ya wanyama kuchinjwa au vile watumishi walivyoshindwa kuingia ofisini wakisema mkurugenzi usivuke, mkurugenzi usivuke, mkurugenzi usivuke?Wengine wakawa wanasema yule hamumuwezi kumloga kwa kuwa amewaolea dada yenu, ukimloga shemeji yako wewe mjomba utalea mwenyewe wapwa zako. Kwa wasambaa shemeji halogwi
[email protected]( Matini hii inapatikana pia katika ukurasa wa facebook wenye jina la Adeladius Makwega.)