Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Jenista Mhagama katikati akimsikiliza mkazi wa kijiji cha Mtyangimbole Halmashauri ya Madaba wilayani Songea Akwilina Mhagama ambaye ni mnufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini anayepokea ruzuku ya fedha kutoka mfuko wa maendeleo ya jamii nchini(Tasaf) alipotembelea Halmashauri ya Madaba kwa ajili ya kuona miradi ya kiuchumi iliyoibuliwa na wanufaika wa mpango huo,kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Jenista Mhagama,akikagua nyumba ya mkazi wa kijiji cha Mtyangimbole Halmashauri ya wilaya Madaba Akwilina Mhagama ambaye ni miongoni mwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini
Baadhi ya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika kijiji cha Mtyangimbole Halmashauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Jenista Mhagama(hayupo pichani) wakati Waziri Mhagama alipowatembelea na kuzungumza na wanufaika hao.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Jenista Mhagama,akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mtyangimbole Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma…
…………………
Na Muhidin Amri,Songea
WANANCHI wanaonufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na mfuko wa maendeleo ya jamii nchini(Tasaf)mkoani Ruvuma,wameaswa kutumia vizuri fedha wanazopokea kwa kubuni miradi na kuanzisha shughuli za kiuchumi ili kujiongezea kipato.
Hayo yamesemwa kwa nyakati tofauti na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Jenista Mhagama, wakati akizungumza na wanufaika wa mpango huo katika kijiji cha Mtyangimbole Halmashauri ya Madaba na Namanguli Halmashauri ya Namtumbo.
Mhagama alisema, hatua hiyo itawezesha kujikwamua kiuchumi na kupunguza umaskini katika familia zao badala ya kuendelea kusubiri ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia Tasaf.
Alisema,serikali ya awamu ya sita kwa mapenzi makubwa imedhamiria kupunguza adha ya umaskini kwa kuendelea kutoa ruzuku ya fedha kila baada ya miezi miwili kwa wananchi wake,lakini ni vyema wanufaika wakajiongeza kwa kuanzisha miradi mingine ya kiuchumi.
Mhagama ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma alisema,utekelezaji wa mpango huo ni wa serikali na wadau wengine wa maendeleo ambao wanaendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa fedha.
Akiwa katika kijiji hicho,ameshuhudia miradi ya ufugaji wa kuku,nguruwe na mbuzi inayotekelezwa na baadhi ya walengwa wa Tasaf ambapo ameridhishwa na miradi hiyo na jinsi wanufaika hao wanavyotumia vizuri fedha za ruzuku katika kupambana na umaskini.
Akizungumza na walengwa wa kijiji cha Namanguli wilayani Namtumbo,Waziri Mhagama amewataka walengwa hao kuhakikisha wanaboresha maisha yao kupitia mpango huo ili kuunga mkono azima ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwakwamua Watanzania na umaskini.
Amewataka wanufaika ambao tayari wamefanikiwa kiuchumi,kujiondoa katika mpango ili kuwapisha watu wengine wenye uhitaji na sifa ya kupata ruzuku.
Kwa mujibu wa Waziri Mhagama,tangu mpango huo ulipoanzishwa jumla ya Sh.bilioni 5.3 zimeshatolewa na serikali kwa ajili ya kuwawezesha wanufaika katika wilaya ya Namtumbo,jambo lililosaidia kuboresha maisha ya wananchi,kupunguza utoro kwa wanafunzi shuleni na watoto kupelekwa kliniki.
Naye Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas,amewataka wanufaika hao kujiuliza juu ya mapenzi makubwa ya Rais Samia namna anavyowapenda kwa kutoa fedha ambazo angeweza kuzielekeza kwenye miradi mingine ya maendeleo.
“mnaopokea fedha hizi za Tasaf ni jukumu lenu sasa kuunga mkono na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan,zitumieni kwa kuboresha maisha yenu na sio vinginevyo”alisema Kanail Laban.
Aidha,amewaonya baadhi ya walengwa kutumia fedha wanazopata kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini kunywea pombe,kwani ni kinyume cha lengo la serikali katika kuanzisha mpango huo.
Mmoja wa wanufaika wa mpango huo kutoka kijiji cha Mtyangimbole wilayani Songea Akwilina Mhagama alisema, ruzuku ya Tasaf imemwezesha kuboresha maisha yake kwa kununua pembejeo kwa ajili ya kilimo na kuanzisha mradi wa ufugaji wa mbuzi.
Ameishukuru Tasaf kwa kumboreshea maisha yake,ambapo ameweza kusomesha watoto na kukarabati nyumba yake kutoka ya nyasi na sasa amefanikiwa kuezeka bati jambo ambalo hakuwahi kulifikiria katika maisha yake.
MWISHO.