……………
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Kutokana na baadhi ya wananchi wilayani Ludewa mkoani Njombe kuishi katika maeneo ya pembezoni na kupelekea watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu katika kutatua changamoto hiyo serikali ipo katika mchakato wa kujenga shule tatu katika kata ya Mlangali, Mavanga pamoja na Ludewa mjini ambayo itajengwa katika eneo la Mdonga.
Akuzungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Mavanga mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema kuwa maeneo mengi ya jimboni kwake huduma za shule zimekuwa chache hivyo baadhi ya wanafunzi hutembea kilometa nyingi kitu ambacho huwafanya washindwe kusoma vizuri na kusababisha utoro.
Amesema kwa sasa amefanikiwa kupatiwa shule hizo tatu lakini ataendelea kuiomba serikali impe shule nyingine tena ili kuhakikisha watoto wote wa jimboni kwake wanapata elimu pasipo kuteseka.
Sanjari na hilo pia mbunge huyo amechangia kiasi cha sh. Ml. 1.4 kwaajili ya utengenezaji wa vitanda katika shule ya sekondari Mavanga, mipira mitatu kwa timu za vijana pamoja na blanket kwa mzee mmoja.
“Serikali inafanya juhudi ya kuhakikisha kiwango cha elimu kinapanda kote nchini, nasi pia tunapaswa kuungana na serikali katika maendeleo hayo hivyo napenda kuwaasa wanafunzi wasome kwa bidii kwakuwa serikali imewekeza fedha nyingi kwao”,. Amesema Kamonga.
Aidha kwa upande wake kaimu Afisa elimu Msingi amekiri kuwepo kwa mchakato huo na kuongeza kuwa kuna wanafunzi wengi ambao hukaa mbali na shule (shule mama) hivyo ujenzi wa shule hizo zitasaidia kuinua kukuza kiwango cha elimu.