Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga akizungumza wakati anafungua mafunzo ya siku tano ya afya moja ambayo yanafanyika kwenye ukumbi wa Tiffany mjini Mtwara yakiwashirikisha watalaam wa sekta mbalimbali kutoka mikoa ya Ruvuma na Lindi
Wataalam mbalimbali wa sekta za afya ya binadamu,mazingira,mifugo,wanyamapori na wanahabari kutoka mikoa ya Ruvuma na Lindi wakipata mafuizo ya afya moja kwenye ukumbi wa Tiffany mjini Mtwara.
Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO Stella Kiambi akizungumza kwenye mafunzo ya afya moja mkoani Mtwara.
…………………………..
Mafunzo ya Timu za Afya Moja za utayari wa kukabiliana na dharura za milipuko ya magonjwa yamefunguliwa mjini Mtwara.Mafunzo hayo ya siku tano ambayo yanafanyika kwenye kumbi wa Hotel ya Tiffany, yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Wataalamu wanaopata mafunzo hayo ni maafisa maliasili,mifugo,wanyamapori,watalaam wa mazingira,madaktari wa binadamu na wanahabari kutoka wilaya za Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi na wilaya za Nyasa na Namtumbo mkoani Ruvuma.
Akizungumza kabla ya kufungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenarali Michael Mumanga ameitaja dhana ya afya moja inakutanisha watalaam na wadau kutoka sekta mbalimbali husasan sekta ya afya ya binadamu,Wanyama,kilimo na mazingira ili kutekeleza usalama wa afya moja duniani.
“Dhana ya afya moja inatumika zaidi kwa sababu vimelea vingi vinavyosababisha vimelea vya magonjwa kwa binadamu vinatoka kwa Wanyama,maambukizi haya hutokea binadamu anapoingilia makazi ya Wanyama bila tahadhari’’,alisisitiza Meja Jenarali Mumanga.
Hata hivyo amesema katika nchi za Afrika hali ni hatarishi zaidi kwa sababu zina mapori makubwa ambayo yanakaribiana na makazi ya watu mfano Bonde la Kongo ni kitovu cha magonjwa ya milipuko kama ebola na homa ya bonde la ufa.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa watalaam katika afya moja hivi sasa ni ajenda ya dunia nzima kwa sababu inapunguza gharama katika kushughulikia matishio ya magonjwa ya milipuko na vimelea mbalimbali vinavyoweza kutoka kwa Wanyama na kwenda kwa binadamu.
Kwa upande wake Dr.Vayan Laizer Mwakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi akizungumza kwenye mafunzo hayo amelitaja lengo la mafunzo ya afya a ni kuimarisha uelewa wa kila mdau na kujenga timu moja ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na vimelea vya maradhi.
Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo na kwa kutumia rasilimali chache zilizopo ni vema kufanyakazi kama timu ili kukabiliana na magonjwa yanayotoka kwa Wanyama.
“Kama tunavyojua zaidi ya asilimia 70 ya magonjwa yanayoambukiza binadamu yanatoka kwa Wanyama,hivyo tunatumia mwamvuli wa afya moja ili kujenga uelewa wa kila mmoja na hatimaye kupunguza athari kwa jamii na kuhakikisha binadamu anakuwa salama’’,alisisitiza Dr.Laizer.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Stella Kiambi alisema afya moja inajumuisha watalaam wa afya ya binadamu,wanyama wa porini na wanaofungwa na mazingira kwa ujumla kufanya kazi pamoja na kwamba kila mmoja kutekeleza majukumu yake kulingana na taaluma yake.
Dr.Mary Kitambi ni Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya,akizungumza kwenye mafunzo hayo amesisitiza ni vema kuzuia magonjwa kutoka kwa Wanyama kwa kutumia afya moja ambapo amesema serikali imeamua kuwaleta wataalam Pamoja ili kujenga uelewa na kuwasiliana kukabiliana na dharura za milipuko ya magonjwa.