Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Ushindani wa kibiashara FCC, Bw. William Erioh akizungumza katika kikao cha pamoja katika ya FCC na Chama cha Mawakala wa Forodha TAFA kilichofanyika kwenye ofisi za FCC jijini Dar Es Salaam kulia ni Makamu wa rais wa chama cha mawakala wa forodha Nchini –TAFFA, Alhaji Waheed Saudin.
Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Ushindani wa kibiashara FCC, Bw. William Erioh akimsikiliza Makamu wa rais wa chama cha mawakala wa forodha Nchini –TAFFA, Alhaji Waheed Saudin wakati akizungumza katika kikao hicho.
Baadhi ya maofiza wa FCC wakiwa kwenye kikao hicho.
Baadhi ya wanachama wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania TAFA wakiwa kwenye kikao hicho.
Serikali kupitia tume ya ushindani wa kibiashara nchini FCC imesema itaendelea kudhibiti uingizwaji wa bidhaa bandia pamoja na uzalishaji wa ndani lengo likiwa ni kukuza uchumi shindani hasa katika soko la Afrika mashariki.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Ushindani wa kibiashara FCC, Bw. William Erioh katika kikao baina ya Tume hiyo pamoja na Chama cha Mawakala wa Forodha Nchini TAFFA kilicholenga kutoa Elimu kuhusu udhibiti wa bidhaa bandia.
“Kwetu sisi wanasheria wanasema kutoakujua sheria siyo utetezi sasa nyinyi mnafanya kazi ya kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa niaba yenu lakini pia kwa niaba ya wamiliki wa kampuni mnazozifanyia kazi mnatakiwa mjue sheria mbaimbali zinazohusika na kusimamia shughuli zenu katika uingizaji wa bidhaa,” Amesema Bw. Erio.
Ameongeza kuwa ili msijekujikuta mnaingia kwenye matatizo ya kuvunja sheria katika shughuli zenu na wale mnaowaingizia bidhaa zao ni muhimu tupeane elimu na kuhakikisha mnaelewa na kufanya kazi katika misingi ya sheria na taratibu zilizowekwa.
“Ni vizuri ninyi mkaelewa hizi sheria ili muwe ndiyo kinga ya kwanza mtu anapokupa bidhaa ili uingize nchini mwetu kazi yako ya kwanza ni kuhakikisha kwamba bidhaa hiyo siyo bandia;” Amesema Bw. Erio.
Ameongeza kwamba hivi karibuni zimekamatwa jezi za Simba na Yanga najua miongoni mwenu kuna watu walihusika kuhakikisha zinaingia kwa sababu wale walionazo huko nje wanatumia ninyi mawakala kuingiza bidhaa hizo nchini.
“Kwa kufanya hivyo vilabu vipepoteza mapato yake lakini pia serikali imepoteza kodi yake ambayo ingekusanywa kupitia bidhaa hizo na fedha hiyo kuleta maendeleo. kazi yenu ya kwanza mnapopata mizigo ya kusafirisha kuja nchini mhakikishe bidhaa hizo siyo bandia,” Amesema Bw. Erio
Pamoja na mambo mengine Erioh amesema tume hiyo inakusudia kufanya marekebisho ya sheria ya alama za bidhaa ya mwaka 1963 hatua hiyo imekuja kutokana na ukuaji wa teknolojia.
Ametanabaisha kwamba huu ni wakati muafaka kwa mawakala wa Forodha kama watendaji au watumiaji wa sheria ile kama kuna eneo ambalo linahitaji kurekebishwa waseme ili katika marekebisho yajayo nalo liwekwe ili muweze kufanya biashara na kuingiza mizigo yenu vizuri na wananchi wapate huduma ambayo ni rafiki kwao.
Kwa upande wake Makamu wa rais wa chama cha mawakala wa forodha Nchini –TAFFA, Alhaji Waheed Saudin amesema watahakikisha wanashirikiana na taasisi nyingine za serikali katika kudhibiti uingizwaji wa bidhaa bandia na kuondoa makandokando yatakayojitokeza.
Tume ya ushindani Nchini FCC ni taasisi ya serikali na imeanzishwa kwa mujibu wa sheria ya ushindani namba 8 ya mwaka 2003 lengo ni kulinda ushindani wa biashara na kumlinda mlaji dhidi ya mienendo gandamizi na potofu.