NA: HUGHES DUGILO.
Irene Thomas Ndunguru ni mhitimu wa mafunzo ya Umeme katika Chuo cha VETA cha Jijini Mbeya miaka nane iliyopita na kupata cheti chake cha Ufundi Stadi Daraja la tatu (Level III).
Maono yake ya kuwa fundi umeme mwenye uwezo wa kufanya kazi zake yeye mwenyewe yalianza kuonekana akiwa bado binti mdogo alipokuwa akisoma katika shule ya msingi Ikulu iliyopo Jijini Mbeya na kuwa mdadisi wa vifaa vya umeme ambapo pia alikuwa akijaribu kutengeneza vifaa vinavyotumia umeme pale vinapopata hitilafu.
Alimaliza masomo yake ya Sekondari katika Shule ya Ilomba na baada ya hapo safari rasmi ya kukamilisha ndoto yake ya kuwa fundi umeme ilikamilika kwa kujiunga na Chuo cha VETA cha Jijini Mbeya.
Irene anasema kuwa VETA iliikamilisha ndoto zake kwa kumpatia ujuzi ambao leo hii amekuwa akijivunia kwa kuwa na uwezo wa kufanya kazi zake kwa weledi mkubwa uliopelekea hadi kuaminika na kufanya kazi kwenye miradi mikubwa ikiwemo kuweka mtandao wa umeme katika Chuo cha VETA cha Wilaya ya Mbarali kilichowekewa Jiwe la Msingi Agosti 8,2022 na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Kati ya mafanikio ambayo najivunia ni kufanya kazi mbalimbali zikiwemo za Serikali ikiwemo katika Chuo cha VETA Mbarali ambacho Mheshimwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweka Jiwe la Msingi wiki hii. Lakini pia nimefanya kazi katika jengo la halmashauri ya Mbeya Vijijini”
“Naamini kitu kinachopelekea kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo miradi ya Serikali ni utendaji kazi mzuri ikiwemo kumaliza kazi kwa wakati katika ule muda unaotakiwa kwa kuzingatia ubora” amesema Irene.
Anaongeza kwa kusema VETA imekuwa kama Mlezi katika maisha yake kwa kumuimarisha na kumshika mkono ukiachia mbali ujuzi aliopata lakini bado ameendelea kufanya kazi mbalimbali za taasisi hiyo.
“Kwangu mimi VETA ni mzazi maana tangu nimefika chuoni mpaka namaliza masomo yangu katika ngazi zote nilizopita wamekuwa wakinishika mkono hata kufikia kuniamini na kuweza kunipa kazi za Chuo kufanya. Mimi naiona VETA kama mzazi”
“VETA haimuachi mtu wakati wote wanakufuatilia na kama kuna mahali wanaona wanaweza kukusaidia basi wanakupa kipaumbele cha kwanza. Pia wana utaratibu mzuri wa kumfuatilia mwanafunzi wao aliyehitimu masomo katika VETA popote alipo na wanakua na taarifa zao na kuendelea kuwasaidia” ameongeza.
Irene amewashauri watanzania wote hususani wazazi kuona uwepo wa vyuo vya VETA nchini kuwa fursa kubwa ya ukombozi wa fikra za vijana kiuchumi katika mapambano ya kujikomboa na ukosefu wa ajira ambapo amesema kuwa kiwango bora cha elimu kinachotolewa na VETA kitapelekea kujiajiri wenyewe na kuweza kuendesha maisha yao mahala popote ndani na nje ya Tanzania.