Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es salaam –ACP Muliro Muliro akizungumza na waandishi wa habari kuhusu namna wanaimarisha ulinzi na usalama katika mkoa wa Dar es salaam
Baadhi wa waandishi wa habari ambao wamehudhuria katika mkutano huo.
…………………..
NA MUSSA KHALID
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limesema linaendelea na operasheni maalum kali ya kuzuia vitendo vya kihalifu maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.
Akizungumza mapema leo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es salaam –ACP Muliro Muliro amesema hali ya kiusalama kwa Jiji la Dar es salaam inazidi kuimarika kutokana na wananchi kuendelea kutoa taarifa mbalimbali za wahalifu,hivyo Polisi wamekuwa wakizingatia maadili, weledi na kuzitunza siri za wananchi.
Aidha Kamanda Muliro amesema amewaomba wananchi kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi ikiwa ni pamoja na kutekeleza falsafa ya ulinzi shirikishii li kuzuia vitendo vya kihalifu
Katika hatua nyingine Kamanda Muliro amesema Katika kuelekea mchezo wa Simba na Yanga Jumamosi Agost 13 mwaka huu Jeshi hilo litachukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo hivyo amepiga marufuku kwa mtu yeyote kwenda na silaha uwanjani isipokuwa vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo
‘Usalama utaimarishwa kwa kiwango cha juu. Ni marufuku kwa mtu yeyote kwenda na silaha uwanjani isipokuwa vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo. Tunawatoa hofu mashabiki watakaofika kushuhudia mchezo huo kuwa ulinzi ndani na nje ya uwanja utakuwa umeimarishwa kwa kiwango cha juu’amesema Kamanda Muliro
Hata hivyo Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam limetoa tahadhari na onyo kali kwa mtu au watu watakaojihusisha na vitendo vya kihalifu ndani au nje ya uwanja kwani wakibainika watawachukulia hatua za kisheria.