Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akihutubia wananchi katika uwanja wa Mwl. Julius Nyerere Mjini Morogoro katika kilele cha siku ya wakulima Nanenane Kanda ya MasharikiWaziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akiangalia ndege nyuki inayotumika kunyunyizia dawa shambani katika banda la bodi ya sukari katika uwanja wa Mwl. Julius Nyerere Mjini Morogoro katika kilele cha siku ya wakulima Nanenane Kanda ya MasharikiWaziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akiangalia kilimo cha Umwagiliaji kwa njia ya mvua katika moja ya kitalu cha Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni katika uwanja wa Mwl. Julius Nyerere Mjini Morogoro katika kilele cha siku ya wakulima Nanenane Kanda ya Mashariki.Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akipata maelezo juu ya kilimo cha kahawa katika banda la Halmashauri ya wilaya ya Lushoto katika uwanja wa Mwl. Julius Nyerere Mjini Morogoro katika kilele cha siku ya wakulima Nanenane Kanda ya Mashariki.
.,……………………
Na Mwandishi wetu
Serikali imetoa rai kwa wadau wa kilimo kuendelea kutambua Ubunifu na Teknolojia mpya zinazooneshwa katika maonesho ya Nanenane ili kuweza kuzikuza na kuzisambaza kwa walengwa wakiwemo Wakulima, Wafugaji na Wavuvi
“Maonesho ya Nanenane yawe ni kitovu cha teknolojia mpya (innovation hub) kwa kuhakikisha kuwa wadau wote wa Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi wanashiriki Maonesho haya, ili kuonesha na kujifunza teknolojia zote zinazotoa majawabu ya changamoto za Sekta hizo,”
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene alipokuwa akihutubia katika kilele cha maonesho ya siku ya Nanenane kanda ya Mashariki yaliyofanyika Uwanja wa Mwl. Julius Nyerere Mjini Morogoro kwa niaba ya mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Sote tunatambua mchango mkubwa wa Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika kuchangia pato la Taifa, ajira, usalama wa chakula na malighafi za viwandani. Ndiyo maana kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu inasema “Ajenda ya Kilimo ni Biashara, Shiriki Kuhesabiwa kwa Mipango Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Waoneshaji wanatakiwa kuhakikisha kuwa takwimu na taarifa sahihi zenye ulinganifu kuhusu teknolojia na bidhaa wanazoonesha zinakuwepo ili ziweze kuwasaidia walengwa kufanya maamuzi sahihi, alisema Waziri”
Aidha Maonesho ya Nanenane yatumike kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuvutia wawekezaji wengi.
Amefafanua kila ngazi kwa maana ya Kanda, Mikoa, Halmashauri na Wadau wengine ifanye tathmini kwa kuangalia mambo mbalimbali ikiwemo hali ya ushiriki na uhalisia wa teknolojia zinazooneshwa kama zinatumika katika maeneo wanayotoka.
Naye naibu waziri wa kilimo Mhe. Anthony Mavunde amesema bajeti ya kilimo imetoka billioni 294 (2021-2022) mpaka kufikia billioni 954 kwa mwaka wa fedha (2022-2023). Wizara ya kilimo tumejipanga kuleta mapinduzi ya kweli katika kufikia ajenda ya 2030 kwa ushirikiano wa wadau wote kuikuza sekta ya kilimo kufikia 10%.
“Bajeti ya umwagiliaji imepanda kutoka billioni 46 ya mwaka wa fedha uliopita hadi kufikia billioni zaidi ya 400 kwa mwaka huu wa fedha (2022-2023). Mikakati ni kuwa na mfumo mzuri wa Umwagiliaji na utekelezaji wake umeanza kwa kupitia mabonde yote 22 ya umwagiliaji ili kufanya upembuzi yakinifu na usanifu ili tuanze kufanya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo hayo, alisema Naibu waziri.”
Amebainisha katika Utafiti bajeti imepanda kutoka billioni 11.7 kwenda billioni 40 ili kuviwezesha vituo vya utafiti kuja na mbegu bora na mbegu ambazo zinastahimili ukame, sambamba na kujengea uwezo vituo vyetu hasa katika maabara za kupima afya ya udongo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma A. Mwasa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kurudisha pembejeo kwa wakulima. Kupitia ruzuku hiyo mkulima hata nunua kwa bei ya kawaida bali kutakuwa na punguzo ili kumuwezesha mkulima azalishe kwa tija.
“Maonesho haya yana umuhimu mkubwa na yanatoa elimu kubwa kwa wakulima, tumedhamiria kuichukua teknolojia tuliyoipata kuihamishia vijijini alisema mkuu wa mkoa wa Morogoro.”