Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wakala wa Meli TASAC Bw. Abdikaim Mkeyenge akipokea zawadi mara baada ya kutembelea banda la Mamlaka ya Bandari katika maonesho ya Kilimo Nanenane yaliyomalizika leo kwenye uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Abdikaim Mkeyenge akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo katika banda lao la maonesho.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Abdikaim Mkeyenge akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo katika banda lao la maonesho.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Abdikaim Mkeyenge akiwa katika banda la shirika hilo na baadhi ya wafanyakazi.
Afisa Mwandamizi Udhibiti Huduma za Bandari Bw. James Mbwilo akimuelezea CACP Mwamini Rwamtali Kamanda wa Polisi Kikosi cha TAZARA wakati alipotembelea katika banda la TASAC leo kwenye maonesho ya Kilimo ya Nanenane yaliyomalizika leo kwenye uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya.
……………………………..
Katika kutekeleza Ajenda ya 10/30 Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania-TASAC limetoa wito kwa wafanyabiashara na wakulima wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kuendelea kutumia Bandari za Tanzania pamoja na bandari kavu ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za usafirishaji wa mazao hayo.
Bandari kuu za Dar es Salaam,Tanga, Mtwara, Kigoma na Mwanza zimekuwa zikisafirisha kwa ufanisi mkubwa shehena za mizigo mbalimbali ikiwemo mizigo ya wakulima inayoingia na kutoka nchini. Bandari hizi na nyinginezo ndogodogo kisheria zipo chini ya udhibiti wa TASAC.
Akizungumza wakati wa Maonesho ya Wakulima Nanenane Afisa Mwandamizi Udhibiti Huduma za Bandari Bw. James Mbwilo amesema katika kuchochea ajenda ya Ukuaji wa Maendeleo ya Kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, TASAC imekuwa ikidhibiti huduma za bandari na kutoa leseni kwa Bandari Kavu (ICDs) zinazopokea mzigo wa makasha.
Aidha, alieleza kuwa Bandari Kavu zinasaidia kupunguza msongamano kwenye Bandari Kuu ya Dar es Salaam na kusaidia wakulima kuagiza pembejeo na kusafirisha bidhaa kwa uharaka na gharama nafuu.
“Lengo la TASAC ni kumsaidia mkulima aliyeagiza pembejeo kutoka nje ya nchi ama kusafirisha mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwenda nje ya nchi kufika kwa wakati na gharama nafuu”, alisema Bw. Mbwilo.
Akifafanua zaidi, Bw. Mbwilo alisema kuwa, TASAC pia ina jukumu la Kudhibiti Huduma za Bandari na Usafiri wa Majini ambapo shirika kisheria linadhibiti watoa huduma kama waendesha bandari, waendesha bandari kavu, mawakala wa meli, mawakala wa forodha, wakusanyaji/ watawanyaji shehena (consolidators/ deconsolidators), wapimaji makasha (Gross Mass Verifiers- GMVs) na watoa huduma ndogondogo bandarini (Miscellaneous Port Services Providers- MPS).
Akiongelea suala la usalama katika vyombo vya usafiri majini, Afisa Mkaguzi wa Vyombo vya Usafirishaji Majini, Bw. Maulid Nsalamba alisema kuwa TASAC ina wajibu wa kuhakikisha vyombo vya kusafirisha mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi vimesajiliwa na ni salama ili kuchochea ufanisi na uzalishaji zaidi.
“Tunakagua vyombo vya usafiri majini na kwa chombo ambacho kimekidhi vigezo tunakipa leseni ya ubora na kuendelea kukifuatilia katika shughuli zake za kila siku”, alisema Bw. Maulid.
Aidha, TASAC inasimamia mitaala ya mafunzo ya Mabaharia inayotolewa na Chuo cha Bahari cha Dar es Salaam (DMI) ili kuhakikisha vyombo vya usafiri majini vinaendeshwa na wafanyakazi wenye utaalamu unaotakiwa.