Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mtaa Tanzania (TALGWU) Bw. Rashid M. Mtima, Mratibu wa Taasisi ya Public Service International (PSI) Dkt. Everline Aketch, viongozi wa Dampo la Pugu Kinyamwezi wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kuhifadhi taka ngumu.Wafanyakazi wa kuhifadhi taka ngumu wakitekeleza majukumu yao bila kuvaa vifaa vya kufanyia kazi ikiwemo glovu pamoja na viatu vya kazi (Buti).Wafanyakazi wa kuhifadhi taka ngumu katika Dampo la Pugu Kinyamwezi wakipewa vitendea kazi kwa ajili ya kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mtaa Tanzania (TALGWU) Bw. Rashid M. Mtima (kutoka kulia), Mratibu wa Taasisi ya Public Service International (PSI) Dkt. Everline Aketch wakiingia katika Dampo la Pugu Kinyamwezi jijini Dar es Salaam.
…………………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mtaa Tanzania (TALGWU) kwa kushirikiana na Taasisi ya Public Service International (PSI) imewataka wadau mbalimbali kutoa ushirikiano katika kuhakikisha wafanyakazi wa kuhifadhi taka ngumu wanakuwa katika mazingira rafiki wakati wakitekeleza majukumu yao.
Kwa kutambua umuhimu wa wafanyakazi wa kuhifadhi taka ngumu Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mtaa Tanzania (TALGWU) na Taasisi ya Public Service International (PSI) wametoa msaada wa vitendea kazi kwa wafanyakazi wa Dampo la Pugu Kinyamwezi na wakusanya taka ngumu katika soko la buguruni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam na wafanyakazi wa kuhifadhi taka ngumu katika Dampo la Pugu Kinyamwezi na Buruguni Sokoni, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mtaa Tanzania (TALGWU) Rashid M. Mtima, amesema kuwa wakati umefika kwa taasisi na wadau mbalimbali kutoa msaada wa vifaa na vitendea kazi kwa wahifadhi wa taka ngumu kutokana wanafanya kazi katika mazingira magumu.
“Wanapaswa kupewa ushirikiano kwa kuwapatia vifaa ikiwemo glovu, vazi la kazi, viatu vya kazi waweze kufanya kazi zao katika mazingira rafiki na kuepukana na mlipuko wa magonjwa” amesema Bw. Mtima.
Bw. Mtima amesema kuwa TALGWU inatambua umuhimu wanaofanya kazi ya kukusanya na kuhifadhi taka ngumu, kwani wengine ni wanachama wao kupitia makampuni zinazosimamia kazi ya kusafisha mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameeleza kuwa wafanyakzazi wa serikali za mitaa inajumilisha halmashauri zote nchini, huku taka ngumu zote za jiji la Dar es Salssm zikipelekwa kuhifadhiwa katika Dampo la Pugu Kinyamwezi.
Amefafanua kuwa TALGWU kupitia PSI wana malengo ya kuona kwa namna gani wanaboresha mazingira ya kazi katika shughuli za kusimamia taka ngumu kuanzia majumbani mpaka eneo la kuhifadhia.
‘Suala la kusimamia taka ngumu liwe kwa kila mtu hapa nchini na kuona kwa namna gani tunaweza kusaidia katika kuhifadhi, taka sio jambo la kubeza, hivyo kila mmoja tuna kila sababu ya kulisimamia” amesema Bw. Mtima.
Hata hivyo wahifadhi taka ngumu katika Dampo la Pugu Kinyamwezi wameiomba serikali kuweka huduma ya afya katika eneo hilo jambo ambalo litawasaidia pale watakapo pata changamoto.
Wamesema ni vizuri wadau mbalimbali wakajitokeza kwa ajili ya kuwapatia vifaa vya kufanyia kazi kutokana asilimia kubwa wanafanya kazi hiyo bila vitendea kazi na kuhatarisha afya zao.
Wameishukuru Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mtaa Tanzania (TALGWU) na Taasisi ya Public Service International (PSI) kwa kuwapatia vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao.