Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduz (CCM) Ndugu Daniel Chongolo ameitaka Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi kuweka malengo kwa kila Mkurugenzi, Makatibu Tawala wa Mikoa kuhakikisha wanayatambua maeneo yote na kuyawekea programu ya kila mwaka yapimwe baada ya miaka mitatu maeneo yote yatakuwa yamepimwa na kupatiwa hati.
Chongolo ametoa kauli hiyo leo tarehe 5 Agosti, 2022 alipotembelea ujenzi wa shule ya Sekondari katika kata ya Mamsera wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro ambapo alisema kuwa.
Alisema kuwa, kupatikana kwa hati ya maeneo hayo itasaidia yasiingiliwe na kuondoa migogoro isiyo ya lazima hivyo ni lazima kuwekwe programu ya kuhakikisha maeneo yote ya huduma kama shule, Afya ofisi za Serikali na maeneo mengine ya michezo yanapimwa na kuhifadhiwa.
“Hapa mmesema mmechukua eneo kidogo la shule ya msingi na jingine mmenunua kutoka kwa wananchi bila ya kuyapima na kuyaweka kwenye hati ya shule na Halmashauri wakaihifadhi hiyo hati itatokea siku moja kuwa na watoto watakaokuja kusema kiamba chetu kinafika mpaka hapa na kwa sababu hela alichukua baba na hayupo wajukuu wataanzisha mgogoro utakaosumbua watu watakaokuwepo” alisema Katibu Mkuu Chongolo.
Katibu Mkuu alisema kuwa, ni lazima tuwe na uchungu na Ardhi iliyoifadhiwa kwa ajili ya maendeleo ya watu wote hivyo tuilinde kama mboni ya jicho ili badae iwasaidie kuleta matokeo kwenye yale matumizi yatakayokuwa yamepangwa katika maeneo hayo na hiyo ndio kazi ya watumishi na watendaji wa Serikali lazima waweke alama kwa kufanya jambo la tofauti.
“Hatuwezi leo eneo kama hili linamiundombinu mizuri na eneo la kisasa lakini tukiulizwa nani anamiliki eneo hili tunaanza kunyoosha kidole halmashauri lakini hati huna akitokea mjanja hapa akapima kwa siri akachukua hati kesho akituondoa haya madarasa na miundombinu hii hatupati hasara kwa uzembe wetu wa kutopima maeneo na kuyaweka kisheria?” Chongolo alihoji
Alisema kuwa, hawawezi kufanya mambo kwa utamaduni wa zamani sasa hivi wajanja ni wengi tutakuja kujikuta shule za Serikali zinamilikiwa kwenye Ardhi za watu binafsi na halitakuwa sawa kwani kama shule ni ya Serikali ni lazima imilikiwe kwenye Ardhi ya Serikali.
“Nimeona majengo bora na yenye kiwango katika shule hii ya Sekondari lakini kunachangamoto ya eneo la uwanja wa michezo ni lazima mtafute eneo ambalo mtajenga uwanja wa michezo ili vijana na wanafunzi washiriki kikamilifu katika michezo hilo nalo ni somo” alisema Chongolo.
Chongolo alisema kuwa, Serikali inawajibu wa kuwahudumia wananchi na kazi ya ccm ni kufwatilia jinsi huduma zinavyowafikia wananchi hivyo wanataka miundombinu bora itakayowarahisishia wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
#Chongolokazini
#Kaziinaendelea