Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Doyasisi ya Masasi Mchungaji Linus Buriani kushoto akimuangalia samaki aina ya Kampongo mwenye uzito wa kilo 10 wanaopatikana katika mto maarufu wa Ruvuma unaotenganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji,kulia ni mvuvi Zamda Ismail.
Jengo la wazazi lililojengwa kwa msaada wa wadau wa maendeleo shirika la Tanzania Development Trust(TDT)la nchini Uingereza na shirika la Eucanaid la Ubelgiji katika kijiji cha Marumba Halmashauri ya Nanyumbu mkoani Mtwara kwa gharama ya zaidi ya Sh.milioni 22 ambalo limesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa wanawake wa Marumba.
Mwakilishi wa mashirika ya Tanzania Development Trust(TDT)la nchini Uingereza na shirika la Eucanaid la Ubelgiji mchungaji Linusi Buriani wa pili kushoto na mwakilishi maalum wa shirika la Uecanaid la Ubelgiji Edgar Thielinann wa tatu kushoto na David Gibbons wa shirika la Tanzania Development Trust(TDT) wa nne kushoto waliosimama, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji cha Marumba Halmashauri ya wilaya Nanyumbu mkoani Mtwara baada ya kukabidhi jengo la wazazi lililogharimu zaidi ya sh.milioni 22.
Mwakilishi wa mashirika ya Tanzania Development Trust(TDT)la nchini Uingereza na shirika la Eucanaid la Ubelgiji nchini Tanzania Linus Buriani kushoto akizungumza na baadhi ya akina mama wa kijiji cha Marumba wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara,wa kwanza kulia Edgar Gibbons kutoka nchini Uingereza na wa pili kulia mwenyekiti wa seriali ya kijiji cha Marumba Jay Hokololo.
……………………………….
Na Muhidin Amri,
Nanyumbu
KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha na kuimarisha huduma za kijamii hapa nchini,wadau wa maendeleo Shirika la Tanzania Development Trust(TDT) na Eucanaid,wamejenga na kukabidhi jengo la wazazi kwa serikali ya kijiji cha Marumba wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
Akipokea jengo hilo ambalo limegharimu zaidi ya Sh.milioni 22 katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika jana mwenyekiti wa kijiji cha Marumba Jay Hokololo, amewashukuru wadau hao kwa msaada huo wenye lengo la kuboresha sekta ya afya katika kijiji hicho.
“nawashukuru sana wafadhili wetu TDT na Eucanaid kupitia Baba mchungaji Linus Buriani kwa kutujengea jengo hili muhimu kwa ajili ya matumizi ya wajawazito ambalo lisaidia sana kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kwa akina mama”alisema Hokololo.
Alisema, hata katika nchi nyingi zilizoendelea Duniani zimefanikiwa sana kiuchumi kutokana na uwekezaji uliofanywa kwenye huduma za kijamii kama vile afya na elimu kama inavyofanya serikali ya Tanzania inayongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Aliongeza kuwa, kupatikana kwa jengo hilo na hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa miundombinu katika sekta ya afya kwa wananchi wa kijiji cha Marumba ambacho kinapakana na nchi jirani ya Msumbiji.
Akikabidhi jengo hilo kwa serikali ya kijiji mwakilishi wa TDT na Eucanaid Tanzania Linus Buriani alisema,awali wakati wanatekeleza mpango wa miaka mitatu ya kwanza walibaini tatizo kubwa katika kijiji cha Marumba ni mama wajawazito kupenda kujifungulia nyumbani.
Kwa mujibu wa Buriani, hali hiyo ilitokana na utamaduni uliokuwepo kwa muda mrefu na imani potofu kuwa, mwanamke anapojifungua nyumbani anaonekana shujaa jambo ambalo siyo sahihi na salama kwao.
Aidha alisema, baadhi ya wanawake wajawazito walilazimika kujifungulia nyumbani,kwa sababu zahanati yao ilikuwa na chumba kimoja cha kujifungulia ambacho kutokana na kuwa karibu na vyumba vya kutolea huduma nyingine za matibabu hakukuwa na usiri wa kutosha.
Alisema,wanawake wajawazito wanahitaji huduma bora na salama ya uzazi,hivyo kama wadau wa maendeleo wataendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kuboresha huduma katika sekta ya afya na huduma nyingine za kijamii.
Buriani amewaomba wanawake wajawazito,kuwa na tabia ya kuhudhuria kliniki mara kwa mara wakati wote wa ujauzito ili kufahamu hali za afya zao na wajifungue kwenye vituo vya kutolea huduma na siyo kubaki nyumbani kwa ajili ya usalama wao.
“akina mama wanatakiwa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma wakati wote wa ujauzito wao ili waweze kujifungulia sehemu salama badala ya kubaki nyumbani, jambo ambalo siyo sahihi sana”alisema Buriani.
Katika hatua nyingine,wadau hao wamekabidhi vyumba vinne vya madarasa,matundu ya vyoo vya wanafunzi na walimu katika shule ya msingi Marumba.
Pia wamefunga umeme jua(solar), wametoa vifaa vya ofisini(Stationery)mashine ya kuprint mitihani,kompyuta na matenki mawili ya kuhifadhia maji ambapo msaada huo umepunguza uhaba wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi na mahitaji mengine kwa shule hiyo.
Muuguzi kiongozi wa zahanati hiyo Frank Nankoko alisema, kwa sasa idadi ya wajawazito wanaojifungulia nyumbani imepungua kutoka 20 hadi 5 kwa mwaka na hali imetokana na kuwepo kwa mazingira mazuri na salama wakati na baada ya kujifungua.
Alisema,jengo hilo limesaidia kushawishi wajawazito kupenda kujifungulia zahanati na kuwepo kwa sheria ndogo inayomtaka mjamzito anayejifungulia nyumbani kutozwa faini ya Sh.50,000.
Baadhi ya wanawake waliokutwa wakipata huduma ya matibabu katika zahanati hiyo,wameishukuru serikali na wadau hao kujenga jengo hilo ambalo limewavutia na kushawishi wajawazito kwenda kujifungulia zahanati na katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Zabibu Twalibu alisema, katika chumba cha awali changamoto kubwa ilikuwa kukosa usiri wakati wa kujifungua kutokana na muingiliano wa watu wengine wanaofika kupata huduma katika zahanati hiyo.
Ameiomba serikali kupitia wizara ya afya kuongeza idadi ya watumishi na vitanda kwa ajili ya kujifungulia,kwani vilivyopo ni viwili na havitoshi kuhudumia wajawazito wanaofika kwa ajili ya huduma ya kujifungua.