NA BALTAZAR MASHAKA, KAHAMA

MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga kupitia Kata ya Kilago,Khamis Mgeja amesema uchaguzi wa ndani wa CCM unaofanyika sasa unalenga kupanga usajili  mpya wa viongozi kwa uchaguzi mkuu wa  2025.

Amesema uchaguzi huo wa viongozi wa CCM kuanzia ngazi za mashina hadi taifa,sasa umefikia ngazi ya kata na lengo lake kubwa ni kuhakikisha kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao baada ya kuchagua viongozi wenye sifa,waadilifu na wenye uwezo wa kuwatumikia wananchi.

Mgeja aliyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa CCM Kata ya Kilago uliofanyika jana sambamba na uchaguzi wa viongozi wa kata hiyo ambapo alipita bila ya kupingwa katika nafasi ya ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM mkoa kupitia kata hiyo.

Katika uchaguzi huo Mgeja alipigiwa kura 120  na wajumbe wa mkutano huo na hivyo kutangazwa mshindi wa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho ngazi ya Mkoa kutoka Kata ya Kilago, anapotoka.

 Aidha msimamizi uchaguzi huo Hamisa Kalinga ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Bulyanhulu, Halmashauri ya Msalala,alisema kuwa uchaguzi huo umefanyika vizuri na kuwasifu wanachama kwa utulivu tagu mwanzo wa hadi mwisho wa uchaguzi.

Mwansiasa huyo mkongwe baada ya matokeo amesema chaguzi za ndani ya CCM  zinaendelea  vizuri  na demokrasia imetamalaki vizuri chini ya uongozi bora na imara  uliotukuka  wa Mwenyekiti wa CCM, Mama yetu Samia Suluhu  Hassan na  kuhakikisha kila mwanachama  anapata haki  ya kugombea.

“Nawaomba sana wanachama wote wa CCM nchini    tumpongeze na  tumuunge mkono mwenyekiti wetu wa taifa na wasaidizi wake kwa namna wanavyokiendesha Chama, sote ni mashahidi hakuna mwanachama anakosa haki ya kugombea na kuchagua kiongozi anayemtaka,”alisema Mgeja.

Pia kuelekea uchaguzi mkuu ujao Mgeja amewasihi na  kuwataka wale wote ambao hawakubahatika kupata nafasi kutokata tamaa kwani CCM bado ina fursa nyingi kwa wanachama wake kupata uongozi katika nyadhifa mbalimbali siku zijazo.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kilago, Hungwi Mabula amekisifu chama hicho kwa kutoa fursa  na haki kwa kila mwanachama wake kugombea nyadhifa mbalimbali na hivyo kuleta usawa na kuondoa manung’uniko kwa wanachama wake.

Wakati huo huo Mkutano Mkuu wa Kata ya Kilago umempongeza   Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha na kutekeleza miradi mingi ya maendeleo nchini  pamoja na kuwa namba moja katika kuhangaika kutafuta fedha za miradi ya maendeleo  kwa ajili ya wananchi .

Wajumbe hao wamesema Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa ameleta miradi mingi nchini ikiwemo ya ujenzi wa madarasa 15,000 na kuhakikisha mwanafunzi kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita anasoma bure hali itakayowapa mwamko wananchi wengi hasa wa pembezoni kuwapeleka watoto wao shule.