Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
BAADHI ya wananchi wilaya ya Kibaha wameungana na mkuu wa mkoa wa Pwani ,alhaj Abubakari Kunenge kujinasibu kwamba, wamejipanga kuwa sehemu ya mafanikio makubwa kwenye Zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika agost 23 mwaka huu.
Akizungumza na wananchi na baadhi ya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini Mjini Kibaha , Kunenge alisema mkoa huo ulibahatika kati ya vituo 13 nchini iliyofanyika sensa ya majaribio kufanya majaribio kwenye kata ya Pangani Mtaa wa Muheza .
“Kulikuwa na mafanikio katika majaribio hayo ,tuliweza kusimamia Zoezi hilo kikamilifu na kwa hakika tulifanikiwa hivyo tunavyosema tunamaanisha kwani tumejiandaa vizuri mno kwa kutumia teknolojia ya kisasa (kishkwambi ) kurahisisha uhifadhi wa taarifa “
Vilevile alieleza ,mkoa na wilaya umejiwekea mikakati kuanzia vitongoji ,kata,wilaya na mkoa kutoa elimu ya umuhimu wa sensa kupitia mbinu mbalimbali.
“Watendaji 143 wameudhuria mafunzo ili kupata uelewa wa kusimamia Zoezi la sensa,;”Pamoja na vikao viwili vya kamati ya sensa mkoa vimefanyika “
Kunenge alifafanua, mafunzo mbalimbali ya Uelewa kuhusu usimamizi wa Zoezi hilo yalianza kutolewa kuanzia ngazi ya halmashauri na wilaya ambapo yatakuwa kwa siku 19 huku Jumla ya washiriki 5,549 wananufaika na mafunzo hayo wakiwemo makarani zaidi ya 4,000, wasimamizi wa maudhui 478 na wasimamizi wa Tehama133.
Anaeleza, wanaendelea kuhamasisha jamii kuanzia ngazi ya vitongoji ,kata ,wilaya kupitia mikusanyiko , wajasiriamali,makundi ya vijana ,bodaboda ,makongamano ,maeneo ya ibada ,matamasha na ligi za michezo ,kutembea kata kwa kata na mikutano na viongozi wa dini .
“Kifupi kila wilaya imebeba suala la sensa kama agenda ya kila siku ili kuhakikisha tunafanikiwa ,Na nachukua fursa hii kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuliona hili kwani itasaidia shughuli za kimaendeleo kufanyika kwa usawa na kupanga mipango mizuri ya maendeleo”
Kunenge pia alikumbusha wananchi ambao hawajachanjwa chanjo ya Uviko19 wajitokeze kuchanja ili kujikinga na ugonjwa huo.
Kwa upande wa Wakazi wa Mailmoja Kibaha akiwemo Joseph Kazimiri,Anna Siha na Yusuph Seif Walisema wapo tayari kuhesabiwa na Kuwa mabalozi wa wengine kuhamasisha kushiriki kwenye sensa.
Nae Askofu Emmanuel Mhina alisema ,kamati hiyo ilianza kipindi kirefu kufanya maandalizi ya kongamano hilo na hadi sasa wanaona kuna mwelekeo mzuri.
“Tunaona kuna mafanikio makubwa hadi hapa tulipofikia mwitikio ni mkubwa hivyo tunaamini kuwa siku ya sensa wananchi watajitikeza kuhesabiwa”alisema Mhina.
Mchungaji wa Kanisa Anglikana Kibaha Mkoani Pwani Exavia Mpambichile aliwataka Waumini na wakazi wa Mkoa huo kuzingatia maagizo ya Serikali na kujitokeza wakati wa Sensa Ili kupatikana takwimu sahihi itakayofanikisha Serikali kupanga bajeti stahiki .
Alieleza kuwa, viongozi wa dini wamelibeba Zoezi hili watahakikisha linafanikiwa kwa kiasi kikubwa.