Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Holle Makungu akizungumza leo tarehe 3.8.2022 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya utekelezaji katika kipindi cha mwezi April hadi Juni 2022.
…………………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanikiwa kufatilia kutekeleza miradi 12 yenye thamani ya bilioni 3.7 katika sekta ya ujenzi, elimu, afya pamoja na barabara.
Akizungumza leo tarehe 3.8.2022 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya utekelezaji katika kipindi cha mwezi April hadi Juni 2022, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Holle Makungu, amesema kuwa miradi 10 ilikuwa na mapungufu ikiwemo kuchelewa kukamilika kwa mujibu wa mkataba.
Bw. Makungu amesema kuwa kuchelewa kukamilika kwa miradi kumesababishwa kuongezeka kwa gharama ikiwemo vifaa visivyo kidhi ubora pamoja na manunuzi kuwa na bei kubwa zaidi ya soko.
“Eneo la utendaji au utoaji huduma linalalamikiwa kwa na vihatarishi vya rushwa, TAKUKURU hufanya uchambuzi wa mfumo ili kubaini iwapo kuna mianya ya rushwa na mifumo katika sekta za mapato pamoja na ujenzi” amesema Bw. Makungu.
Hata hivyo amebainisha kuwa kamati ya urasimishaji wa makazi haina uelewa na kupelekea kumpatia fedha nyingi mzabuni tofauti na kazi aliyofanya na kusababisha mchakato kuwa na mapungufu kuanzia hatua ya uelimishaji kwa wananchi huhusiana na zoezi uchangiaji.
Amesema kuwa Manispaa imewaachia wananchi zoezi wakati hawana utaalamu wa urasimishaji jambo ambalo limesababisha kuleta mkwamo katika urasimishaji wa makazi.
“Mfano kuna michoro ambayo mkandarasi ameiwasilisha Manispaa ili ipatiwe idhini hadi sasa Manispaa haijampatia Mkandarasi mrejesho ya kile alichokiwasilisha, TAKUKURU imejipanga kufanya kikao cha pamoja ili kujadili namna bora ya kukabiliana na mapungufu yaliyojitokeza” amesema Bw. Makungu.
Hata hivyo amesema kuwa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ni Wakala chini ya Wizara ya Ujenzi imebainika kuna kuwepo wa madeni makubwa kwa taasisi zinazotoa huduma TEMESA na kusababisha kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi., kwani TEMESA wanadai zaidi ya Tsh bilioni tisa kutoka kwa wateja wake waliowahudumia.
Amesema kuwa kutokana na deni hilo TAKUKURU Mkoa wa Temeke imefanya kikao cha pamoja na wadau na kutoa mapendekezo yanayowezesha taasisi zinazopata huduma zinalipa madeni wanayodaiwa ili kuipa nguvu TEMESA.
“Mpaka sasa baadhi ya taasisi zimeshaanza kulipa madeni yao TAMESA jambo ambalo linaleta matumaini katika kuendea kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa” amesema Bw. Makungu.
Katika hatua nyengine ameeleza kuwa katika kipindi cha robo ya Julai hadi Septemba mwaka huu TAKUKURU Mkoa wa Temeke imejipanga kuendelea kuimarisha jihudi za kuzuia rushwa kwa kufatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika vita dhidi ya rushwa kupitia vyenzo mbalimbali za uelimishaji.
“Tunaendelea kufatilia makusanyo na uwasilishaji wa mapato yanayotokana na mashine za POS na kuchukua hatua stahiki kwa wale watakaobainika kufuja mali za umma” amesema.
Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Temeke kutoa ushirikiano katika kuzuia rushwa na kutoa taarifa za rushwa jambo ambalo litasaidia kuleta maendeleo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali