WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa taasisi za umma na za binafsi zishirikiane na Serikali katika mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi ili kuokoa maisha ya wanawake na kuepuka madhara yatokanayo na saratani hiyo.
“Kama wanavyosisitiza wataalam wetu wa afya, saratani ya shingo ya kizazi inatibika na inaweza kuepukika endapo itatolewa elimu ya kutosha yenye lengo la kuwasisitiza wanawake kupima afya zao mara kwa mara ili kupata tiba stahiki.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa saratani ya shingo ya kizazi inagharimu maisha ya wanawake nchini, mwaka uliopita wanawake wasiopungua 9,219 walifanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti na ya shingo wa kizazi ambapo 364 walionekana kuwa na dalili za awali za saratani na wengine 26 waligundulika kuwa na saratani hiyo.
Amesema hayo leo (Jumapili, Julai 31, 2022), aliposhiriki NBC Dodoma Marathon katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma. Ameipongeza benki hiyo kwa jitihada zake katika kuchangia upimaji na matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake nchini kwa kutoa shilingi milioni 200 zilizopatikana kutokana na mbio hizo.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kufanya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma za matibabu na uchunguzi wa kibingwa na ubingwa bobezi wa ugonjwa wa saratani.
“Hatua hii ni pamoja na kutekeleza mradi wa kusimika mashine ya PET/CT Scan kwa gharama ya shilingi bilioni 18.2 pamoja na ujenzi wa jengo jipya la huduma ambalo sasa limefikia asilimi 96.