…………..
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAZIRI wa Madini Dkt Dotto Biteko amewatoa hofu wadau wa madini ya Tanzanite wawe na utulivu katika kipindi hiki cha mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya rasimu za kanuni mpya za biashara ya madini hayo.
Waziri Dkt Biteko akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite katika wa mji mdogo Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, amesema mchakato huo unaendelea hivyo haina haja ya kutoa maneno ya malalamiko ya kanuni mitandaoni zikiwa hata bado hazijapitishwa.
“Tunachohitaji ni maoni yenu ili mfahamu tunapokwenda kwa lengo kuweza kuboresha kanuni lakini maneno ya malalamiko yameanza je kesho nani atakuwa na ujasiri wa kuja kwenu kuchukua maoni,”amesema Dkt Biteko.
Amesema kuwa hazuiwi kutunga kanuni na ikiwa na matatizo yatarekebishwa lakini lengo ni kushirikishana ili kuweka utaratibu wa kudumu.
Amesema kuwa lengo la kuwashirikisha wadau wa sekta hiyo ni kutoa maoni ya rasimu za kanuni za biashara ya Tanzanite ni kuwa pamoja katika utungaji wa kanuni ili isilalie upande mmoja hivyo ni vyema wachimbaji na wafanyabiashara wa Tanzanite wakawa watulivu katika kutoa maoni hayo.
Pia, Dkt Biteko amemtaka mkandarasi wa ujenzi wa jengo la soko la madini ya Tanzanite (Tanzanite City) linalojengwa katika mamlaka ya mji mdogo Mirerani kukamilika kwa wakati.
Amesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa soko la madini ya Tanzanite ulioanza kutekelezwa Mei 22, mwaka huu na kutegemewa kukamilika Mei 2023 unagharimu takribani sh.bilioni 5.4, unaojengwa na shirika la nyumba la Taifa (NHC) chini ya mkandarasi Goodlack Masika.
Meneja wa shirika la nyumba za Taifa (NHC) mkoa wa Kilimanjaro Juma kiyalamba amesema amepokea maelekezo hayo atayafanyia kazi katika kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati ili kuweza kufikia lengo la serikali kuwepo kwa soko la madini mkoani Manyara.
Afisa madini mkazi wa madini (RMO) Mirerani, Fabian Mshai amesema ofisi inapendekeza utolewaji wa leseni ya kitalu C kwa mzabuni aliyeshinda ili kazi zianze kufanyika jambo litakalosaidia kupunguza athari zitokanazo na uvamizi wa wachimbaji wasio rasmi.
“Pia ofisi inaomba maboresho ya miundombinu ya huduma za kijamii kama umeme, maji na mawasiliano kwenye maeneo mbalimbali nje na eneo la Mirerani ili kuwa na mazingira rafiki kwa uwekezaji wenye tija kwa sekta ya madini na Taifa kwa ujumla,” amesema RMO Mshai.