MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinanana amemshauri Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camilius Wambura kufanya tathimini ili kuona uwezekano wa kupunguza idadi ya askari wa usalama barabarani ambao wanalalamikiwa na wananchi kusababisha kero.
Kinana ametoa ushauri huo jana akiwa katika mwendelezo wa ziara yake katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambapo wananchi wa maeneo mbalimbali ya mikoa ya Songwe na Mbeya wamelalamikia idadi kubwa ya askari wa barabarani ambao wamekuwa wakiwasimamisha mara kwa mara, kutaka fedha ambazo hata hivyo hawatoi stakabadhi yoyote.
Malalamiko hayo ya wananchi yaliendelea kuibuka hata katika kikao cha ndani cha wanachama wa CCM Mkoa wa Songwe ambapo mmoja ya wanachama hao, dereva wa magari ya kubeba abiria maarufu kama Costa, kutoa malalamiko mbele ya Kinana akidai wamechoka kusimamishwa mara kwa mara na trafiki na kila wanaposimama wanatoa sh. 2,000 kwa kila kituo.
Akijibu malalamiko hayo Kinana alisema kwanza anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua IGP Wambura. “Nampongeza Rais kwa kumtea IGP mpya, nina hakika ni IGP mwadilifu, mchakazi na hodari.
“Lakini namuomba na kumshauri atazame wingi wa trafiki mijini, kila baada ya muda mfupi unasimamishwa na trafiki, wenye magari hawaendeshi kwa raha, hivyo nimsihi IGP afanye tathimini kuhusu uwepo wa trafiki wengi kwenye miji yetu, wamekuwa wengi sana kila ukitembea kidogo unasimamishwa, kilomita moja unakuta trafiki.
“Namuomba IGP afanye tathimini watu wapumue, watu biashara zao zinaharibika kwa sababu ya kuambiwa paki pembeni, tunaheshimu umuhimu wa usalama nchini, lakini tunakerwa na kuambiwa paki gari pembeni. Namuomba IGP, naheshimu na natambua uwezo wake mkubwa, lakini afanye tathimini je, kuna umuhimu wa kuwa na idadi kubwa ya trafiki barabarani?´alihoji Kinana.
Pamoja na hayo Kinana alisema katika ziara yake amepokea malalamiko mengi ya wananchi wakilalamikia idadi ya trafiki na katika kushughulikia malalamiko hayo, ametoa ushauri huo kwa IGP Wambura kuangalia uwezekano wa kufanya tathimini kuhusu uwepo wa idadi ya trafiki barabarani.
Akizungumzia ushauri huo wa Kinana, IGP Wambura alisema ni mzuri sana na ameupokea.
IGP Wambura alisema ushauri huo una afya kwa maendeleo na kwamba anakwenda kuufanyia kazi ndani ya taasisi yake.