Na Joseph Lyimo
WAKATI hivi sasa Serikali ipo kwenye shughuli ya kuhakikisha wananchi wake wanapata chanjo ya UVIKO-19 ili kuondokana na janga la maradhi hayo, bado kuna baadhi ya imani na dhana potofu iliyojenga miongoni mwa wananchi mbalimbali juu ya chanjo hiyo.
Pamoja na Serikali kupitia wataalamu wa afya wameendelea kutoa elimu juu ya manufaa ya chanjo ya UVIKO-19, ila bado kuna baadhi ya wananchi wanaendelea kupotosha shughuli hiyo ili hali hawana elimu ya chanjo.
Miongoni mwa fikra na imani pofotu zinazotolewa hivi sasa ni kuwa wanaopata chanjo ya kujikinga maambukizi ya UVIKO-19, hawatakuwa na uwezo wa kupata watoto imesababisha hofu kwa baadhi ya watu kutojitokeza kupata chanjo hiyo.
Mkazi wa kata ya Kaloleni wilayani Kiteto, Athuman Khalfan anasema imani potofu hiyo imesababisha baadhi ya watu wa eneo hilo kutoshiriki chanjo hiyo, japokuwa wataalam wa afya wanafika kuelimisha watu.
“Tunamshukuru mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Dkt Malikiadi Mbota na wataalamu wa afya kwa namna wanavyotoa elimu na kuwaelimisha watu kuwa chanjo ya UVIKO-19 haina madhara ya kusababisha ugumba na kutopata watoto,” amesema Khalfan.
Amesema awali wananchi walishindwa kushiriki ipasavyo kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani elimu ya uchanjaji hawakuipata walijazwa hofu kuwa wanaopata chanjo hiyo hawatapata watoto katika maisha yao yote kumbe siyo ukweli.
“Imani potofu zinazotia hofu wananchi kuhusu chanjo ya UVIKO-19, kutokuwa na elimu ya chanjo na umbali wa vituo vya kutolea chanjo na maeneo waliopo wananchi ndizo sababu kuu za wengi wao kutojitokeza kupata chanjo ila hivi sasa tunafuatwa mtaa kwa mtaa na nyumba kwa nyumba,” anaeleza Khalfan.
Mkazi wa kata ya Partimbo wilayani Kiteto, Isack Parmelo anaeleza kuwa awali yeye alishindwa kuchanja chanjo ya UVIKO-19 kutokana na kuelezwa na watu kwamba chanjo hizo zina madhara kiafya na zinasababisha wanaume kutosababisha ujauzito kwa wanawake.
“Baada ya wataalamu wa afya kunipa elimu na kuelewa juu ya faida ya chanjo ya UVIKO-19 na mimi ni mtu wa kusafiri mno mara leo Arusha, kesho kutwa Dar es salaam, niliamua kuchanja na sikupata madhara,” anasema Parmelo.
Parmelo anaeleza kwamba hajapata madhara yoyote kiafya tangu amepata chanjo ya UVIKO-19 aina ya jonson jonson hivyo kinachozungumzwa ni uzushi wenye kuwatia hofu wananchi kwani hivi sasa mke wake ni mjamzito.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, Dkt Malikiadi Mbota, amesema kuwa walipambana na imani na fikra potofu kwa kutumia wataalamu wa afya, viongozi wa dini, wazee wa kimila naa watu maarufu kwenye kata na vijiji, wamefanikiwa kutoa elimu na hivi sasa wananchi wanapata chanjo ya UVIKO-19.
“Shughuli ya uchanjaji inafanyika hivi sasa kwa wingi kwani wananchi wanajitokeza na kupata chanjo ya UVIKO-19 ikiwa ni njia mojawapo ya kujikinga na maradhi hayo, baada ya kupata elimu kwani muitikio ni mkubwa mno,” anasema Dkt Mbota.
Mkuu wa mkoa wa Manyara (RC), Charles Makongoro Nyerere ametaka elimu kutolewa kwa wananchi ili kuondoa dhana potofu zilizojengeka miongoni mwao na kusababisha baadhi ya wananchi wasishiriki kupata chanjo ya UVIKO-19.
“Natoa wito kwa viongozi wote wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji, viongozi wa dini, wazee wa kimila na jamii kwa ujummla kushirikiana kuhakikisha wananchi wanapata chanjo ya UVIKO-19 ,” anasema RC Makongoro.
Makongoro anasema viongozi wa dini wakitumia nyumba za ibada na kutoa elimu kwa waumini wao waondokane na mawazo potofu waende kuchanja ili kupata kinga ya UVIKO-19 kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha inalinda afya zao.
Anaeleza kuwa viongozi wa kimila wana ushawishi mkubwa pia kwa jamii katika kuhakikisha wanawaelimisha wananchi wa maeneo yao kuwa Serikali haina nia mbaya katika kutoa chanjo ya UVIKO-19 hivyo jamii iepuke dhana potofu.
Mratibu wa UVIKO-19 kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMA, Dkt Mwanahamis Hassan anasema kuna umuhimu wa wananchi kupata chanjo hiyo, kwa kuwa ugonjwa upo japokuwa wagonjwa wanafikia hatua ya kulazwa siyo wengi kama ilivyo kuwa awali.
Dkt Mwanahamis anasema takwimu zinaonyesha kwamba tangu ugonjwa huu uliporiptiwa nchini hadi sasa jumla ya watu 34,002 walithibitika kuwa na Uviko 19 na watu 803 wamepoteza maisha.
Hata hivyo, hivi karibuni Serikali imeeleza kuwa kati ya Watanzania 3,509 waliolazwa kutokana na UVIKO-19 kwa kipindi cha Septemba 2021 mpaka JulaI mwaka huu, wagonjwa 3,337 sawa na asilimia 95 hawakuwa wamepata chanjo.
Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Dk Beatrice Mutayoba anasema takwimu hizo zimeendelea kushuhudia namna ambavyo chanjo imesaidia kwani bado Watanzania wanaugua kwani takwimu za Juni 4 mpaka Julai Mosi vimeonyesha kuwepo kwa visa vipya 352 kutoka visa 161 kwa kipindi cha Mei 5 hadi Juni 3.
Anaeleza kwamba chanjo ndiyo kinga pekee kwani wanaolazwa wengi hawajachanja kati ya wagonjwa 3,507 waliolazwa kutoka Septemba mwaka jana mpaka Julai mwaka huu imebainika wagonjwa 3,337 sawa na asilimia 95 hawakuchanja.
“Kati ya vifo 96 vilivyotokea katika kipindi hicho, 93 viliwahusisha wale ambao walikuwa hawajapata chanjo sawa na asilimia 96.07 hii inatuthibitishia umuhimu wa kupata chanjo kama kinga dhidi ya ugonjwa huu,” anaeleza Dkt Mutayoba.
Mpaka sasa mikoa iliyoonyesha kufanya vizuri dhidi ya kiwango cha juu cha uchanjaji ni Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam ambapo mpaka sasa takribani watu 1.5 milioni wamechanja ikiwa malengo ni kuwafikia watu milioni 2.5.