Mwenyekiti wa Tanzania Long Distance Truck and Bus Drivers Association –TLDT Hassan Dede akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam akitolea ufafanuzi kuhusu suala la mgomo wa madereva.
Mwenyekiti wa Tanzania Long Distance Truck and Bus Drivers Association –TLDT Hassan Dede akizungumza kwa njia ya simu na Rais Mstaafu wa Chama cha Madereva Zambia na Mwenyekiti katika Baraza la Ushauri SADC Bob Ndalama.
………………….
NA MUSSA KHALID
Mwenyekiti wa Magari yanayokwenda masafa Marefu Tanzania –TLDT Hassan Dede amewataka madereva kuepukana na migomo bali waendelee kutoa huduma kwani madai yao yatawasilishwa serikalini ili kupatiwa ufumbuzi.
Dede ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari akitolea ufafanuzi kuhusu suala la mgomo wa madereva ambapo amesema ni vyema wakatulia kwani serikali kupitia Waziri Mkuu inashughulikia masuala yao.
Mwenyekiti huyo amesema wamepanga kukutana na Waziri Mkuu au kiongozi yeyote wa serikali kuwasilisha madai yao ili waweze kujadili na kusaidiana kupeleka changamoto za madereva hao hivyo wategemea majibu kabla ya mwisho wa mwezi huu.
‘Mimi kama mdau wa achalia mbali na uenyekiti kama mdau wa taifa hili ninayependa maendeleo sote tunafahamu serikali kupitia Waziri Mkuu ameshatoa tamko kwamba shughuli ziendelee hivyo tupo makuni na tupo sambamba na viongozi wetu wa ngazi za juu kuwasikiliza na kuwatii wanachokisema nasema magari yaendelee kutoa huduma mgomo hakuna’amesema Dede
Mwenyekiti huyo wa TLDT akizungumza kwa njia ya Simu na Rais Mstaafu wa Chama cha Madereva Zambia na Mwenyekiti katika Baraza la Ushauri SADC Bob Ndalama amesema wamezungumza na viongozi wa vyama wasizuie gari lolote badala yake wayaache yafanye kazi.
Amesema hawawezi kusimamisha magari bila serikali au kuonana na watu wanaosimamia sekta ya uwekezaji kwani ni jambo linaloweza kusababisha mgogoro kwa serikali hizo.
July,26 mwaka huu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa usimamizi ufanyike kuhakikisha magari yote yaliyokwama katika maeneo mbalimbali nchini hususani mipakani yanaandaliwa utaratibu wa kukwamuliwa na kuendelea na safari huku masuala yao yakiendelea kutafutiwa ufumbuzi.