Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa mshituko na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mtambile, wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, kuwahi kuwa Waziri kivuli wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa na hadi anafariki alikuwa Msemaji wa Masuala ya Ulinzi katika Chama cha Act Wazalendo, Ndugu Masoud Abdallah kilichotokea Kisiwani Pemba Jumatatu 25 Julai 2022.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan amemtumia Salaam za rambi rambi Mwenyekiti wa Chama Cha Act Wazalendo Mheshimiwa Juma Duni Haji kufuatia kifo cha kiongozi wao huyo muandamizi katika chama.
“Tutamkumbuka kwa ucheshi, ukarimu na utayari wake nyakati zote akiwa ni miongoni mwa viongozi waliokuwa mstari wa mbele katika kuunganisha, kuumini maridhiano na mapatano ambae mara zote hata kuwe na jambo ngumu kiasi gani busara zake huwa ni sehemu ya kupatikana suluhu, ni mwanansiasa aliyependa kujichanganya ili kutetea na kusimamia maslahi mapana ya wananchi, tumempoteza kiongozi tegemeo na mwenye utayari katika kuhakikisha Umoja na mshikamano unatamaalaki nchini” Ndugu Samia Suluhu Hassan
Chama Cha Mapinduzi kinatoa pole kwa wana familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu Masoud Abdallah kufuatia msiba huo na kuwaomba kuwa na uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.
Sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.
Shaka hamdu Shaka
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
Itikadi na Uenezi.
Julai 26, 2022