Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania –TFRA Dkt Stephan Ngailo akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam akitoa taarifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluh Hassan kuzindua mpango wa utoaji wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima.
……………………….
NA MUSSA KHALID
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania -TFRA imewataka wakulima nchini kujitokeza kujiandikisha na kujisajili kwenye Ofisi za serikali za vijiji vyao ili waweze kunufaika na mpango wa serikali wa kuwapunguzia makali ya bei ya Mbolea kupitia Ruzuku.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Dkt Stephan Ngailo wakati akitoa taarifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluh Hassan kuzindua mpango wa utoaji wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima.
Dkt Ngailo amesema kutokana na kupanda kwa bei za mbolea katika soko la Dunia na hapa nchini serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 150 kugharamia ruzuku ya mbolea itakayotolewa kwa wakulima wote nchini kwa lengo la kupunguza makali ya bei za mbolea na kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo.
Amesema kuwa Serikali imeamua kutumia Mfumo wa kidigitali kutekeleza mpango wa ruzuku ya Mbolea ili kuongeza ufanisi,kupunguza mianya ya udanganyifu Pamoja na Muda na gharama za Usimamizi.
Aidha Dkt Ngailo amesema kuwa Mbolea zitakazohusika kwenye Ruzuku ni za kupandia na kukuzia ambapo DAP kwa ajili ya kupandia na Urea kwa kukuzia ambazo zote ni takriban Asilimia 50 ya matumizi yote ya Mbolea Nchini.
Dkt Ngailo ameeleza kuwa Mfumo huo utafanya kazi kwa mkulima aliyesajiliwa ataenda kwa mfanyabiashara wa Mbolea aliyesajiliwa Kwa ajili ya kununua Mbolea na kuonyesha namba ya utambulishe aliyopewa wakati wa usajili.
“Ili kuhamasisha matumizi ya Mbolea zinazozalishwa nchini,zinazozalishwa na viwanda vya ndani zitaingia kwenye mpango wa ruzuku kulingana na mahitaji ya soko”amesema Dkt Ngailo
Amesema uuzaji wa mbolea kwa wakulima na malipo ya ruzuku ya mbolea mfumo huo utafanya na makampuni yataingiza na kuzalisha mbolea nchini na kuifungasha katika mifuko yenye uzito wa kilo 25 na 50 ambayo itaandikwa ‘MBOLEA YA RUZUKU’na itachapwa QR Code itakayotolewa na TFRA.
Amesema utekelezaji wa mpango wa ruzuku ya Mbolea utahusisha wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Kilimo,Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea TFRA,Kamati Tendaji ya Ruzuku,Sekratieti za mikoa,Mamlaka ya serikali za mitaa,WAINGIZAJI/wazalishaji wa Mbolea,Mawakala wa Mbolea,Taasisi za Fedha na wakulima.
Pia ameziomba serikali za vijiji,viongozi,watendaji na mabalozi sambamba na maafisa ugani kushiriki kikamilifu katika zoezi la usajili wa wakulima na utoaji wa ruzuku ili kuhakikiha mkulima anafaida jambo litakaloisaidia kukuza uchumi wanchi.