……………………..
Na Sixmund J. Begashe wa MNRT
Wizara ya Maliasili na Utalii imekutana na kufanya mkutano na wadau wa Utalii nchini ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambayo alilolitoa Juni 7, 2022 katika mkutano wa 13 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Jijini Dodoma.
Akifungua mkutano huo Leo jijini Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Balozi Dkt. Pindi Chana amewahakikishia Wadau wa Utalii kuwa Wizara anayoiongoza inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika Sekta ya Utalii ili ichangie kikamilifu katika Uchumi na maendeleo ya Taifa.
Waziri Balozi Dkt.Pindi Chana ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kupunguza wingi wa mifumo ya usajili, malipo ya ada ya leseni na tozo mbalimbali katika Sekta ya Utalii.
“Kama mnavyofahamu, dhamira hii pia inaenda sambamba na uendelezaji wa malengo ya kimkakati ya Programu ya Tanzania – The Royal Tour katika kukuza utalii kadhalika na uhifadhi wa maliasili na malikale zetu”. Amesema.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufikia malengo ya kuongeza idadi ya watalii, mapato, na wigo wa mazao ya utalii kupitia uwekezaji wa shughuli mbalimbali za utalii ili kukuza utalii na kuufanya uwe endelevu.
Kuhusu maoni mbalimbali yaliyotolewa na wadau wa Utalii, Waziri Balozi Dkt.Pindi Chana, ameziagiza Taasisi zote za Wizara ya Maliasili na Utalii kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa ndani ya kipindi cha miezi mitatu ili kuboresha sekta ya Utalii.