Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Mwanza Mhe Kabula Shitobelo akizungumza na wananchi wa kata ya Misungwi.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akizungumza na wananchi wa wilaya ya Misungwi waliojitokeza kwaajili ya uchimbaji wa msingi wa ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Mbela Baadhi ya wananchi wa kata ya Misungwi waliojitokeza kushiriki uchimbaji wa msingi wa ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Mbela.
…………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwenye mazingira rafiki na salama,Mkoa wa Mwanza umeanzisha kampeni ya kupunguza changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa inayoitwa uzalendo kwanza kazi iendelee itakayo wasaidia wanafunzi kusoma vizuri.
Kampeni hiyo imezinduliwa leo jumatatu Julai 25, 2022 katika shule ya msingi Mbela iliyopo Wilaya ya Misungwi Mkoani hapa.
Akizindua kampeni hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, amesema kampeni hiyo ya kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa ina thamani ya Bilioni 238.08.
Amesema watanzania wanapaswa kuwa wazalendo kwa kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuchimba msingi, kusomba mawe ili kuweza kupunguza gharama zitakazosaidia katika kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mbunge viti maalumu Mkoa wa Mwanza Kabula Shitobelo, amesema wazazi wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kuwapeleka watoto wao shule hivyo kufanya idadi ya wanafunzi kuwa kubwa ukilinganisha na vyumba vya madarasa vilivyopo hivyo kupitia kampeni hii nitasaidia tofari 400 kila Wilaya zitakazosaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Misungwi Alexander Mnyeti amechangia Milioni 20 kwaajili ya kuunga mkono ujenzi wa vyumba 25 vya madarasa katika shule ya mbela.
amesema shule ya Mbela ina watoto wengi kuliko shule zote zilizoko kwenye wilaya hiyo, uwezo wa shule ni kubeba wanafunzi 800 lakini idadi ya wanafunzi waliopo kwenye shule hiyo ni 2000 hivyo ujenzi wa Madarasa hayo yatakuwa suluhisho la kudumu na itasaidia wanafunzi kusoma vizuri
Naye Mkuu wa wilaya ya Misungwi Veronica Kessy, amewaomba wananchi kuendelea kujitolea katika kufanya kazi za kimaendeleo hali itakayosaidia watoto kusoma katika mazingira mazuri na hatimae kutimiza ndoto zao.