Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam Ng’wilabuzu Ludigija akizungumza na wenyeviti,watendaji wa mitaa mbalimbali na wakuu wa Idara wa Wilaya hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Amani Mafuru akieleza namna watakavyotekeleza maagizo ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija.
Viongozi na wadau mbalimbali waliohudhuria katika kikao hicho .(picha na Mussa Khalid)
……………………..
NA MUSSA KHALID
Watendaji na wenyeviti wa mitaa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam wametakiwa kufanya jitihada za kusimamia suala la utunzaji wa Mazingira kwenye maeneo yao ili kulifanya jiji hilo kuwa katika hali ya usafi wakati wote.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam Ng’wilabuzu Ludigija ametoa wito huo leo wakati akizungumza na wenyeviti,watendaji wa mitaa mbalimbali na wakuu wa Idara wa Wilaya hiyo ikiwa ni katika kuelekea kufanyika kwa usafi wa kila mwisho wa mwezi.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema usafi wa mwisho wa mwezi huu utafanyika kivingine hasa utalenga kwenye barabara zote zinazozunguka jiji hilo hivyo amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi.
Aidha ametoa onyo kwa wafanyabiashara wadogo maarufu Machinga Wilayani humo wanaorejea katika maeneo waliyoondolewa na kutishia kuwachukulia hatua wenyeviti na watendaji wa Serikali za Mitaa wanaotajwa kuhusika kuwarejesha maeneo hayo yasio rasmi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Amani Mafuru amesema maelekezo yote ambayo ameyatoa mkuu wa Wilaya watahakikisha wanayatekeleza kwa ukamilifu.
Mafuru amewataka watendaji kufanyia kazi maelekezo ya mkuu huyo wa wilaya huku baadhi ya watendaji wa mitaa wakisema kuwa adhma hiyo inawezekana na Dar es salaam ikawa safi
wakati wote.
Naye Kiongozi wa wenyeviti katika jiji la Dar es salaam Ally Mshauri akizungumza kwa niaba ya wenyeviti,amesema kuwa watakwenda kuyasimamia na kutatekeleza maelekezo yote ikiwemo kuwapanga na kuwaondosha wafanyabiashara waliorudi katika maeneo yao.
Katika kikao hicho pia wamehudhuria wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa usalama,Viongozi wa wafanyabiashara,na Kiongozi Shirikisho la Bajaji na Bodaboda,hivyo wananchi wote waanaokaa kulia na kushoto kwenye maeneo ya barabara wametakiwa kujitokeze kwa wingi katika ufanyaji wa usafi mwishoni mwa Mwezi huu.