Muhifadhi Mila Mwandamizi Kijiji cha Makumbusho Dar es salaam Wilberd Lema.
…………………..
NA MUSSA KHALID
Kijiji cha Makumbusho Dar es salaam kimeanzisha program ya kuwafunza mabinti namna ya kwenda kuziangalai familia zao (kuwafunda) ili kuendelea kuuhifadhi utamaduni wa mtanzania.
Hayo yameelezwa na Muhifadhi Mila Mwandamizi Kijiji cha Makumbusho Dar es salaam Wilberd Lema wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ambapo amesema lengo ni kuhakikisha wanaendeleza utamaduni lakini kuondoa changamoto ya watu kupotoshwa.
Lema amesema wameamua kuwafunda mabinti kutokana na kubainika kumekuwa na changamoto mbalimbali kwenye ndoa zao hasa zikitokana na elimu wanayoipata katika sehemu isiyosahihi.
Aidha Muhifadhi huyo mwandamizi amesema Makumbusho kama taasisi inayolinda utamaduni wanafanya program hiyo kwa ajili ya kulinda upotoshaji lakini pia wataanzisha program hiyo kwa wanaume kuwa majasiri.
‘Tumeangalia kwa jamii sasa hivi zimebadilika kuna wakina dada mabinti ambao wanakwenda kwenye ndoa lakini hawajui mambo mengi kwa hiyo tunawatafuta Makungwi ambao wanakuja wanawafunda hao mabinti huduma ya kulipia kwa muda wa wiki nzima sio suala la siku moja ni mpaka wiki nzima ili uelimike vya kutosha ndo uruhusiwe’amesema Lema
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Dar es salaam wakizungumza kwa nyakati tofauti,Mery Rubert mwanafunzi wa mwaka wa pili UDSM pamoja na Medison Eneck wamesema dhamira ya kufundwa ni kutunzwa kwa utamaduni wa mtanzania katika jamii.
Hata hivyo watanzania wametakiwa kuendelea kuuthamini na kuutunza utamaduni wao sambamba na kutembelea kujionea malikale mbalimbali nchini ili kuifahamu historia ya nchi yao.