…………………
Na Sixmund Begashe wa MNRT
Wizara ya Maliasili na Utalii imeeleza kuwa katika mwaka fedha wa 2022/2023 imejipanga kikamilifu kutekeleza vipaumbele 7 vinavyogusa maisha ya wananchi ili waendelee kunufaika na kazi kubwa inayofanywa na Wizara hiyo ya kuhifadhi, kulinda na kusimamia maliasili na malikale pamoja na kuendeleza utalii nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Mhe. Balozi Dkt Pindi Chana alipokuwa akizungumza na waadishi wa Habari Jijini Dodoma kuelezea vipaumbele vya Wizara yake na mikakati mbalimbali iliyowekwa kuwanufaisha wananchi.
Waziri Balozi Dkt. Chana ameeleza kuwa katika mwaka huu wa fedha, Wizara yake imeindhinishiwa na Bunge kutumia kiasi cha jumla ya Shilingi Bilioni 624,142,732,000 ambazo pamoja na mambo mengine zitatumika katika kutafuta suluhisho la kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanayamapori wakali na waharibifu kupitia utoaji wa elimu na vitendea kazi pamoja na kujenga vituo 19 vya kuwathibiti wanyamapori hao hususan tembo, viboko na mamba kwenye maeneo yenye matukio mengi pamoja na kuanzisha matumizi ya mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kupokea taarifa za matukio hayo nchini.
Sambamba na hilo ameeleza kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi na Wizara nyingine za kisekta ili kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi za vijiji ili kuepusha migongano na hifadhi inayotokana na wananchi kuanzisha makazi katika shoroba ambayo ni maeneo ya mapito ya asili ya wanyamapori.
Aidha, Balozi Dkt. Pindi Chana amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara yake imejipanga kikamilifu kuendeleza Programu ya The Royal Tour iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza kasi ya kutangaza utalii kitaifa na kimataifa na kuibua fursa za masoko mapya ya utalii.
Amefafanua kuwa Wizara yake itaendelea kuvitangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii kufikia watalii 5,000,0000 na mapato dola za marekani 6,000,000,000 ifikapo mwaka 2025. “Kuongezeka kwa mapato haya kutaiwezesha Serikali yetu kutoa huduma za msingi kwa wananchi kama vile huduma za afya, elimu, maji na miundombinu.
Aidha, kupitia fedha hizo amesema Wizara yake itakarabati na kuimarisha miundombinu ya barabara, vivuko, huduma za malazi, viwanja vya ndege na maeneo ya huduma za dharula za uokoaji kwa wageni hususan wanaopanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuongeza usalama na kuvutia watalii wengi zaidi waitembelee Tanzania.
“Fedha hizi zitatumika kuboresha miundombinu yetu katika maeneo ya hifadhi, kuibua na kuendeleza mazao mapya ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa fukwe, mikutano na matukio, meli za kitalii, michezo na utamaduni, Kuimarisha shughuli za upandaji miti, mazao ya Misitu na ufugaji nyuki na mnyororo wa thamani wa mazao hayo”. Amesisitiza.
Waziri Pindi Chana.
Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana amebainisha kuwa kupitia fedha hizo Wizara itaimarisha mfumo wa utoaji wa huduma bora za utalii ili kukidhi viwango vya kimataifa na Kuboresha ulinzi na usalama wa rasilimali za maliasili na malikale.
Katika hatua nyingine Waziri Pindi Chana ameeeleza kuwa Wizara yake itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa Maliasili na malikale kwa kuboresha matumizi ya sayansi na teknolojia kwa kununua vifaa vya kisasa vya mawasiliano ili kuwezesha operesheni za doria kufanyika kwa tija na ufanisi zaidi.
Amesema Wizara itaendelea na jitihada za kutangaza maeneo ya malikale katika Gazeti la Serikali kuwa Urithi wa Taifa na kushirikisha jamii kutambua umuhimu wa kuhifadhi, kulinda na kuendeleza malikale ili kunufaika na urithi huo pamoja na kuanza ujenzi wa Makumbusho ya Waheshimiwa Marais Jijini Dodoma ambayo itasaidia kuonesha kwa jamiii mchango wa marais katika nyanja za kijamiii, kisiasa na kiuchumi kwa kipindi walichokuwa madarakani.