Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Biashara pamoja na sehemu ya Maafisa walioambatana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma wakimsikiliza Jaji Mkuu alipokuwa akizungumza na Watumishi hao tarehe 15 Julai, 2022.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian Mkeha akitoa taarifa mbele utendaji kazi wa Divisheni hiyo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha.Majaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Biashara wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma hayupo katika picha).
…………………………….
Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameitaka Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kubuni mbinu mbalimbali ikiwemo kuanzisha Mahakama ndogo za Biashara nchini zitakazowezesha kuharakisha uondoshaji wa mashauri ya biashara yakiwemo ya Wafanyabiashara wadogo popote walipo.
Akizungumza na Watumishi wa Divisheni hiyo tarehe 15 Julai, 2022 jijini Dar es Salaam alipokuwa kwenye ziara ya kikazi, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa Divisheni hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na mazingira ya biashara na uwekezaji.
“Kwa mfano sasa hivi Machinga wameondolewa barabarani na imani kama sasa wanaweza kuwa na madai mbalimbali, kama kungekuwa na Mahakama ya Biashara ambayo ingesikiliza mashauri ya wafanyabishara ndogondogo yatakayoamuliwa kwa muda mfupi na kuwawezesha kuendelea na shughuli zao, hivyo mnavyofikiria kuboresha sheria na kanuni mbalimbali za Divisheni hii msisahau kulipa kipaumbele hili,” amesema Jaji Mkuu.
Kwa upande mwingine, Mhe. Prof. Juma ameitaka Divisheni hiyo kupunguza idadi ya siku za kutoa hukumu kwa mashauri ya biashara kutoka miezi 12 hadi kufikia miezi nane (8).
“Jambo mojawapo tuliloahidi kwenye Mradi wa Benki ya Dunia kuhusu Mahakama ya Biashara ni kuhusu kupunguza idadi ya siku za utoaji wa hukumu na tayari mmeshataja miezi 12, nadhani mmefanikiwa kufikia azma ya Benki ya Dunia kwa sababu wao walisema kwamba mashauri ndani ya miaka mitano (5) ifikapo mwaka 2025 shauri la kibiashara lichukue siku 250 tu, kwahiyo hata hiyo miezi 12 hakikisheni 2025 mnamaliza ndani ya miezi nane, kwahiyo mkifikia hatua hiyo mtakuwa mmefikia lengo la Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania,” ameeleza Mhe. Prof. Juma.
Ameongeza kuwa, ahadi nyingine ambayo imetolewa kwenye Mradi wa benki ya Dunia ni kupunguza idadi ya vituo/mlolongo wa usikilizaji wa mashauri kutoka vituo 38 hadi vituo 21 kwa Mahakama zote ila Mahakama ya biashara inabidi kuangalia uwezekano wa kupunguza zaidi ili kuharakisha uondoshaji wa mashauri yake.
“Vilevile ni muhimu kuwa makini katika kupokea mashauri, msiruhusu kupokea mashauri ambayo hayajakamilika kwa kuwa, yanasababisha mlundikano,” amesisitiza.
Hali kadhalika, Mhe. Prof. Juma amewakumbusha Watumishi hao kuhusu matumizi ya TEHAMA ambapo amesisitiza kuwa mfano katika safari ya kuelekea Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.
“Imefika wakati sasa tunapoelekea Mahakama mtandao kama ni kanuni au sheria zibadilishwe haraka ili kuendana na karne ya sasa. Mfano tabia ya kutumia vitabu vingi vilivyoandaliwa na Wadaawa kuvileta mahakamani vya kufungulia kesi havihitajiki tena, walete nakala laini na Majaji wawekewe ‘screen’ na kompyuta ya kusoma nyaraka hizo mahakamani, hii itawezesha kuikamilisha kaulimbiu yetu ya Siku ya Sheria na safari yetu ya kuelekea Mahakama Mtandao. Kwanza kuandaa vitabu hivyo ni gharama kubwa pengine kuwe na kitabu kimoja kinachowasilishwa kwa ajili ya rejea,” ameeleza.
Naye, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian Mkeha amesema kwa mwaka 2020 Divisheni ya Biashara ilifunga mwaka ikiwa na jumla ya mashauri 527 yaliyosalia. Mwaka 2021 Divisheni hiyo ilisajili jumla ya mashauri 607.
“Katika mwaka wa kazi wa 2021 mashauri 516 yalimalizika. Katika mwaka huo wa kazi wa 2021 Divisheni yetu ilifunga mwaka ikiwa na jumla ya mashauri 618 yaliyosalia. Kwa upande wa mwaka huu wa kazi, kufikia tarehe 14 Julai, 2022 Divisheni ilikuwa imesajili jumla ya mashauri 349 na kumaliza jumla ya mashauri 530. Kwa ujumla mashauri yanayomalizika ni mengi kuliko yanayofunguliwa, jambo ambalo ni ishara nzuri katika harakati za kupambana na tatizo la mlundikano wa mashauri,” amesema Mhe. Mkeha.
Jaji Mkeha ameongeza kuwa, kiwango cha uondoshaji wa mashauri katika Divisheni hiyo kinaridhisha ambapo kuanzia Januari hadi Desemba, 2021 waliondosha mashauri kwa asilimia 85 na kuanzia Januari mwaka huu hadi kufikia tarehe 14 Julai, 2022 wameondosha mashauri kwa asilimia 152.
Aidha, Jaji Mkeha amesema kuwa mpaka sasa, Divisheni hiyo ina jumla ya mashauri 37 yanayosikilizika ambayo ameahidi hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu yatakuwa yamesikilizwa na kutolewa uamuzi.
Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma alianza ziara yake tarehe 13 Julai, 2022 maalum kwa ajili ya kutembelea Divisheni za Mahakama Kuu ambapo alianza kwa kutembelea Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi na Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi. Katika ziara hii Mhe. Prof. Juma amewakumbusha Watumishi wa maeneo hayo Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu isemayo Mapinduzi ya nne ya Viwanja; Safari ya maboresho kuelekea Mahakama Mtandao, hivyo amesisitiza kuhusu matumizi ya TEHAMA katika Mahakama ili kufikia azma ya kuwa Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’ ifikapo 2025.
Katika ziara yake ya siku nne (4) Mhe. Prof. Juma amepanga kutembelea pia Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi na kuhitimisha ziara yake tarehe 20 Julai kwa kutembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeke.