Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Nickson Saimon ‘Nikki wa Pili’ (wa kwanza kutoka kushoto) akipokea msaada wa taulo za kike kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Raising Up Friendship Faundation (RUFF0) Bi. Hilda Ngaja (wa kwanza kutoka kulia) ni Afisa Mradi Bi. Latifa Miraji kutoka RUFFO.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Nickson Saimon ‘Nikki wa Pili’(wa kwanza kutoka kushoto), Mkurugenzi wa RUFFO Bi. Hilda Ngaja, Afisa Mradi wa RUFFO Bi. Latifa Miraji, Mkurugenzi Mwenza na Afisa Maendeleo wa RUFFO Bw. Amos Mhando wakiwa katika picha ya pamoja Mkoani Pwani.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Bw. James Chitumbi akizungumza na jambo Mkaoni Pwani kuhusu umuhimu wa shule za msingi na sekondari kuwa na taulo za kike kwa ajili ya kukabiliana na dharura wakati wanafunzi wa kike wakiwa katika hedhi shuleni.
Uongozi wa Taasisi ya Raising Up Friendship Faundation (RUFF0), Baadhi ya watendaji wa Wilaya ya Kisarawe wakiwa katika kikao na Mhe. Nickson Saimon ‘Nikki wa pili’ Ofisini kwake. (Picha na Noel Rukanuga).
……………………….
NA NOEL RUKANUGA, PWANI.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kuendelea kuwekeza nguvu katika kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto pamoja na kuhakikisha wanasoma katika mazingira rafiki jambo ambalo litawasaidia kutimiza ndoto katika maisha yao.
Akizungumza hivi karibuni Mkoani Pwani wakati akipokea msaada wa taulo za kike kutoka Taasisi ya Raising Up Friendship Faundation (RUFF0), Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Nickson Saimon ‘Nikki wa Pili’ amesema kuwa wanaendelea kuwajengea uelewa wanafunzi kuwa na uwezo wa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya ukatili kupitia program mbalimbali.
Mhe. Saimon ameishukuru taasisi ya RUFFO kwa kuleta taulo za kike katika Wilaya ya Kisarawe, kwani taulo hizo zinakwenda kutatua changamoto kwa wanafunzi katika shule zenye uhitaji wilayani humo.
“Nitakuwa sehemu ya kampeni hii ya kuchangia taulo za kike na katika mikutano yangu nitalizungumzia ili kuwasaidia wanafunzi wa keki kipindi ambacho wanapata hedhi wakiwa shuleni wawe katika mazingira rafiki” amesema Mhe. Saimon.
Akizungumzia kuhusu vitendo vya ukatili wilaya ya kisarawe, ameeleza kuwa idadi ya matukio ya ubakaji yamepungua kwa asilimia kubwa, na hali hiyo imetokana na kufanikiwa kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa ajili ya kuchukuwa hatua.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Bw. James Chitumbi, amesema kuna baadhi ya wanafunzi wapo katika mazingira magumu wakiwa katika kipindi cha hedhi kutokana na kushindwa kumudu gharama za taulo za kike.
“Msaada wa taulo za kike unakwenda kuwasaidia wazazi na wanafunzi wa kike, wataona umuhimu wa kwenda shule bila kuona aibu yoyote kwa sababu kuna vitu ambayo vinawaifadhi wakiwa katika kipindi cha hedhi” amesema Bw. Chitumbi.
Ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wa jambo hilo halmashauri ya kisarawe wanapojenga miundombinu ya shule wanatenga vyumba maalam vya wanafunzi wa kike kwa ajili kujiifadhi wakiwa katika hedhi.
Amebainisha kuwa wakati umefika serikali kutenga bajeti maalam kuwa ajili ya ununuzi wa taulo za kike kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.
“Bajeti ikitengwa iwe na usimamizi, inaweza serikali kuu ikatoa maagizo kwa halmashauri ya Wilaya itenge asilimia ya fedha katika mapato yake kwa ajili ya kununua taulo za kike kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji shuleni” amesema Bw. Chitumbi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya RUFFO Bi. Hilda ngaja, amesema kuwa kupitia kampeni ya kuchangia taulo za kike wanaendelea kutoa msaada katika shule mbalimbali zenye uhitaji kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kike wakiwa katika hedhi.
Bi. Ngaja amesema kuwa lengo ni kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki ya afya na uzazi na kuwasaidia kuepukana na changamoto ya kuomba ruhusa ya kwenda nyumbani wakati wakipata hedhi.
“Tatizo la hedhi linakuja kama dharura, hivyo taulo za kike zitawasaidia wakiwa shuleni na kuepuka usumbufu wa kwenda nyumbani kipindi cha masomo” amesema Bi. Ngaja.
Amesema kuwa katika Wilaya ya Kisarawe wamefanikiwa kwenda katika shule ya msingi na sekondari ya Mfuru kwa ajili ya kuwapa wanafunzi taulo za keki jambo ambalo litawasaidia wakiwa katika hedhi shuleni.
Taasisi ya Raising Up Friendship Foundation (RUFFO) inayopatika pia kupitia website ya www.ruffo.or.tz inaendelea na kampeni ya kuchangia taulo za keki kwa shule zenye wanafunzi wenye uhitaji katika Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Pwani.