Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bravo Group Bi. Angelina Ngalula akizungumza na waandishi wa habari baada ya wadau wa zao la chai kutembelea Soko la Chai linalojengwa jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bw. Nicholaus Mauya akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara ya kutembelea Soko la Chai linalojengwa na Kampuni ya Bravo Group.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania Bw. Teofody Nduguru akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara ya kutembelea Soko la Chai linalojengwa na Kampuni ya Bravo Group.
Wadau wa zao la Chai wakiwa katika picha wakati wa kutembelea Soko la Chai linalojengwa na Kampuni ya Bravo Group jijini Dar es Salaam.
……………………………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kampuni ya Bravo Group inatarajia kufungua soko kubwa la chai hapa nchini jambo ambalo litasaidia kuongeza fursa za uwekazaji pamoja na kuleta ahueni kwa wafanyabiashara na wakulima wa zao la chai.
Imeelezwa soko hilo linatarajiwa kufunguliwa mwaka huu jijini Dar es Salaam na kupunguza gharama za uendeshaji katika viwanda na wakulima zao la chai, ambapo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98.
Akizungumza leo tarehe 13, 7, 2022 baada ya kufanya ziara ya kutembelea Soko la Chai linalojengwa na Kampuni ya Bravo Group jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bw. Nicholaus Mauya, amesema kuwa serikali imeweka mikakati ili kuhakikisha wanaanzisha soko la chai hapa nchini.
Bw. Mauya amesema kuwa kuanzishwa kwa soko la chai hapa nchini ni moja ya hatua kwa serikali katika kuhakikisha wanaendelea kutengeneza mazingira ya rafiki kwa wawekezaji ili kufia malengo tarajiwa.
“Huduma zote zitakuwa zikifanyika hapa nchini kwani awali wakulima walikuwa wanauza chai kupitia soko la Mombasa nchini Kenya na kutumia gharama kubwa za kusafirisha wa bidhaa zao” amesema Bw. Mauya.
Amebainisha kuwa wafanyabishara walikuwa wanasafirisha kotena moja la futi 40 kutoka Mfindi hadi Mombasa kwa gharama ya shilingi milioni nane, lakini kwa sasa gharama za usafirishaji zitapungua na kufikia milioni nne.
Ameeleza kuwa mtaona ni jinsi gani uwepo wa soko litakavyookoa fedha nyingi katika kusafirisha zao la chai wakati soko litakapoaza kufanya kazi hapa nchini.
Bw. Mauya amefafanua kuwa mpaka sasa uzalishaji wa zao la chai ni kilo milioni 37 kwa mwaka, lakini bado wana mikakati ya miaka 10 ya kuendeleza kuongeza uzalishaji hadi kufikia kilo milioni 90.
“Miaka mitatu tayari imepita na sasa tumebakiwa miaka saba, hivyo hadi kufikia mwaka 2030 lengo la mkakati wa kuzalisha zao la chai kilo miloni 90 litakuwa limefanikiwa na kupanua soko letu kwa kiasi kikubwa” amesema Mauya.
Ameeleza kuwa wakifanikiwa kuzalisha kilo milioni 90 kwa mwaka na kuweza kuwashawishi nchi jirani ikiwemo Uganda, Burundi na Rwanda kwa kuleta mazao katika soko la Tanzania litaongeza uzalishaji wa kilo milioni 100 na kufikia kilo milioni 200.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bravo Group Bi. Angelina Ngalula, amesema kuwa Kwa muda mrefu zao la chai ya nchini Tanzania wafanyabiashara wamekuwa wakisafirisha na kupeleka sokoni Mombasa nchini Kenya.
Mwekezaji huyo amesema kuwa kupitia juhudi ambazo zimefanya na serikali zao la chai litakuwa likiuzwa hapa nchini na kuzileta nchi mbalimbali kuja katika mnada.
“Tumeamua kufanya uwekezaji kwa kufungua soko la chai hapa nchini na tayari tumeagiza mitambo mikubwa kwa ajili kuhudumia zao la chai na kwa sasa tupo katika hatua ya mwisho ya kumaliza ujenzi wa soko hili” amesema Bi. Ngalula.
Amesema kuwa wamefikia asilimia 98 za kukamilisha ujenzi wa soko hilo na kuanza kutumia kwa ajili ya mnada wa chai kwa watanzania pamoja na nchi mbalimbali.
Bi. Ngalula ameeleza kuwa waziri wa kilimo Mhe. Hussein Bashe tayari amefanya mazungumza na soko kubwa la mnada wa Chai ambalo lipo Dubai, huku lengo ni kuliunganisha soko hilo na Tanzania.
“Mtu ataweza kununua chai akiwa dubai, lakini chai yake inaweza kuifadhiwa nchini Tanzania, tupo tunatengeneza mtandao mkubwa wa kimataifa” amesema Bi. Ngalula.
Amesema kuwa soko hilo litafungua milango ya wageni kuja hapa nchini kutoka mataifa mbalimbali kwa ajili ya kununua bidhaa ya chai na watoa huduma wataweza kunufaika.
“Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa katika soko hili la chai jambo ambalo litasaidia kuchangia uchumi wetu na kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo” amesema Bi. Ngalula.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania Bw. Teofody Nduguru, ameishukuru Kampuni ya Bravo Groups na serikali kwa mkakati wa kuleta soko la chai nchini Tanzania.
Bw. Nduguru amesema kuwa kuna wakulima wadogo wa zao la chai 32,000 ambao wapo katika wilaya 14 hapa nchini wakiwa wanalima zao la chai na kuwauzia wadau wa viwanda.
“Soko hili linakuja kutatua changamoto ya bei, kwani bei ya majani mabichi ya chai ni ndogo kutokana na gharama kubwa iliyokuwa ikitumiwa na waendeshaji wa viwanda pamoja na wenye masoko” amesema Bw. Nduguru.
Kampuni ya Bravo Group ambayo imefanya uwekezaji wa kufungua soko la chai nchini Tanzania inajiusisha masaula ya usafirishaji pamoja mambo mbalimbali kuhusu bandari.