…………………..
Na Silvia Mchuruza,Muleba, Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge amewahimiza watumishi kufanya kazi kwa weledi mkubwa sana na viwango ili wananchi waweze kupata matunda bora ya Serikali yao.
Ametoa kauli hiyo alipokutana na kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri na kuwaeleza kuwa wakiwajibika na kufanya kazi vizuri wananchi wataipenda na kuzidi kuiamini Serikali yao.
“Unapowajibika kwa dhati kutoka ndani ya moyo wako na kuwajibika ipasavyo hapo utakuwa umewatendea haki wananchi unawatumikia na ndipo wananchi wanavyozidi kuipenda Serikali yao na kuiamini katika kuwaletea maendeleo” amesema Meja Jenerali Charles Mbuge.
Sambamba na hayo amewahimiza watumishi kuwa na umoja na mshikamano ili kuepusha migogoro baina yao na ili waweze kufanya kazi kwa kiwango na ubora unaotakiwa katika kuwatumikia wananchi.
Taarifa iliyosomwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Elias Kayandabila amesema kuwa Halmashauri ya wilaya ya Muleba inakusanya mapato makubwa kupitia vyanzo vitatu kutoka sekta ya uvuvi ambavyo ni tozo za leseni za uvuvi, ushuru wa mazao ya uvuvi na tozo za faini kwa makosa mbalimbali ya uvuvi yaliyokiukwa na wavuvi/wafanyabiashara wa mazao ya samaki.
Pia amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri imekusanya jumla ya Tsh. Bilioni 3.2 kati ya Tsh. Bilion 2.9 zilizokisiwa kukusanywa kupitia mazao ya uvuvi. Aidha Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imekusanya jumla ya mapato Tsh. bilioni 5.8 kati ya hizo Tsh. bilioni 3.2 imekusanywa kutoka kwenye Sekta ya Uvuvi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila ameeleza kuwa kupitia mapato ya ndani Halmashauri imejenga Kituo cha Afya katika kisiwa cha Bumbile kwa kiasi cha Tsh. Milioni 500, kituo ambacho kitaenda kuwanufaisha wananchi hususani wa visiwani kwa kupata huduma za matibabu kwa urahisi kuliko kuja nchi kavu.
Lakini pia amesema kuwa katika suala la kupambana na utoroshwaji wa kahawa za magendo, Wilaya imeendelea kuwaelimisha wananchi juu ya utaratibu mpya wa kuuza kahawa kwa njia ya mnada ambao unakwenda kuwanufaisha wakulima wadogo kupitia zao hilo la Kahawa.