………………………..
Adeladius Makwega-DODOMA
Mwaka 2012 nilifika DW Bonn Ujerumani katika jengo linalorusha matangazo ya Idhaa kadhaa ikiwamo ya Lugha ya Kiswahili ambapo idhaa hii ilianza kazi hizo tangu mwaka 1953.
Nilipofika hapo kwa kuwa ulikuwa msimu wa baridi kali ya Februari, mkuu wa idhaa ya Kiswahili ambaye alikuwa mjerumani alinipatia koti la baridi lenye nembo za Idhaa hii ambalo lilinisaidia mno kupambana na baridi kwa siku za mwanzo.
Nilitafutiwa sehemu yakuishi na maisha yakaanza, niliporudi ofisini siku iliyofuata nilipangiwa kufanya kazi katika chumba kimoja cha mwisho mkono wa kushoto katika ofisi za Idhaa hii.
Hapo palikuwa na dawati lenye meza na viti kadhaa, simu ya mezani, runinga, kompyuta yenye mtandao muda wote na redio inayotumia satalite inayokamata matangazo ya redio zote za kimataifa.
Nilipokuwa nikilifungua dirisha jirani yangu kipindi kisichokuwa cha baridi upepo mwanana wa Mto Rhine ulinipuliza vizuri huku vyombo vinavofanya shughuli zake katika mto huo navyo niliviona kila uchao.
Baada ya siku mbili nilibaini kuwa katika chumba cha ofisi hii sikuwepo mwenyewe bali walikuwapo watu wengine wawili. Nilijiuliza je ni kina nani? Sikupata jibu.
Asubuhi moja macho yangu yalikaribishwa na mama mmoja mrefu wa kadri, mweusi, anayependa kuchana nywele ambaye ni mchangamfu sana. Mama huyu ambaye alikuwa mkweli, muwazi sana, makarimu sana na anayeheshimu dini yake Uisilamu.
“Mwanangu Adeladius, mimi baba yangu alikuwa ni Mkomoro, zamani watu wengi wenye asili ya kwetu walikwenda Zanzibar kutafuta maisha na ndiyo maana nikazaliwa Zanzibar, lakini baada ya mapinduzi nikiwa binti mdogo nikarudi na wazazi wangu Komoro.”