……………………………
Na Faisal Abdul (COSTECH), Dar es salaam.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia (WyEST) inatarajia kuanza mchakato wa mapitio ya Sheria Namba 7 ya mwaka 1986 ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili iendane na wakati wa sasa ambapo mchango wa Maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu inachangia kiasi kikubwa katika maendeleo ya Nchi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia (WySTE), Mhe. Mhandisi Omary J. Kipanga ambaye alimuwakilisha Waziri wa Elimu alipotembelea Banda la COSTECH katika Maonesho ya Kimataifa ya 46 ya Biashara Dar es salaam maarufu kama Sabasaba.
Akizungumza baada ya kutembelea Banda hilo na kujionea tija ya bunifu mbalimbali zilizobuniwa na vijana wa Kitanzania ambao wamewafadhiliwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Tume hiyo Mhe. Kipanga amesema kuwa Sheria namba ya 7 ya mwaka 1986 ya COSTECH wakati Tume inasimikwa rasmi mwaka 1988 hakukua na kipengele cha ubunifu ndani yake hivyo Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) imetoa maagizo ya kupitia Sheria hiyo na sera zake ili kuhakikisha inaendana na mahitaji ya wakati wa sasa.
” Kwenye nyanja ya Ubunifu Taifa la Tanzania limepiga hatua kubwa kwa sasa tunatengeneza bidhaa mbalimbali kupitia bunifu za ndani hivyo nasisitiza bunifu hizi zilindwe na wabunifu wapate stahiki zao na ziwafaidishe na kutengeneza ajira” amesema Naibu Waziri Kipanga
Hata hivyo Mhe. Kipanga ameitaka COSTECH kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuendelea kulijenga Taifa .
” Lengo la bunifu hizi ni kutatua changamoto mbalimbali Nchini kwasababu changamoto zinatofautiana kutoka Taifa moja hadi jingine hivyo tutatumia bunifu zetu za ndani kutatua changamoto hizo” amesema
COSTECH ni miongoni mwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia (WyEST).
“Nimekuja hapa kwa niaba ya Mhe. Waziri, ametemebelea kuona kinachoendelea katika banda hilo kwenye utaratibu wa ukuzaji wa tafiti na maeneo Mengine pamoja na kuona bunifu na wabunifu mbalimbali ambao wamelelewa na COSTECH” ameongeza Mhe. Kipanga
Amesema kuwa Tume ina Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji Sayansi na Teknolojia (MTUSATE) kwajili ya kugharamia shughuli za utafiti na Ubunifu pamoja na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) ambayo huratibiwa ili kuhakikisha tafiti na bunifu zinaweza kulelewa , kukuzwa na kuendelezwa ili zifikie hatu ya ubiasharishaji wa kuwa bidhaa ambazo zitatatua changamoto katika Jamii.