Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) imekipatia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zaidi ya Sh Bilioni 11 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miudombinu katika Taasisi ya Sayansi za Bahari.
Akizungumza mjini Zanzibar mwishoni mwa wiki mara baada ya kutembelea Taasisi hiyo Mhe. Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya kuendeleza baadhi ya miundombinu hiyo ambayo ujenzi wake ulisimama kwa muda mrefu.
Ameongeza kuwa fedha hizo zimepelekwa katika Taasisi hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aligiza fedha zilizopatikana kutokana na Mradi wa HEET kusambazwa nchi nzima ili ziweze kuboresha na kujenga vyuo vitakavyowapatia ujuzi na ajira watanzania.
” Maelekezo ya Mhe. Rais kuhusu fedha za mradi huu ni kusambazwa kwa nchi nzima ili kuboresha na kujenga miundombinu pamoja na kutoa ajira kwa watu mbalimbali, ndio maana tumeleta fedha hizi hapa lakini pia zimekwenda Tabora, Musoma, Mara, Geita Simiyu, Manyara, Tanga na kwingineko” amesema Prof Mkenda
Waziri huyo amekitaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhakikisha kinasimamia kwa weledi fedha hizo ili zifanye kazi ambayo imekusudiwa kwa ubora na viwango vilivyokubalika
Aidha, Prof Mkenda amemtaka Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Prof. Evaristo Riwa kufika katika Taasisi hiyo ili kuona mapungufu ya mradi wa ujenzi wa baadhi ya miundombinu iliyojengwa chini ya usimamizi wa chuo hicho na kurekebisha mapungufu hayo kabla ya kuanza kwa awamu nyingine.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mhe. Suleiman Haroub amesema fedha hizo zilizotolewa zimeamsha matumaini kwa wananchi wanaozunguka Taasisi hiyo kwani baada ya kuona misingi ya miundombinu hiyo imekaa muda mrefu bila kuendelezwa walijua kinachofuata ni kuondolewa katika eneo hilo na kuahidi kushirikiana na Taasisi hiyo kulinda mazingira na miundombinu.
Mbunge wa Jimbo la Kiembe Samaki Mhe. Mohamed Maulid ameishukuru Wizara ya Elimu na Serikali kwa kutoa fedha za uendelezaji wa ujenzi wa miundombinu na kwamba itakapokamilika itakuwa Taasisi nzuri yenye kuzalisha vijana watakaoshiriki katika kuendeleza uchumi wa bluu.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari Mosses Mbiru amesema fedha hizo zinakwenda kukamilisha jengo la utawala na taaluma pamoja na kutekeleza azma ya upanuzi wa shughuli za Taasisi hiyo.