Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga akizungumza na wadau wa utalii ambao wanafanya utalii wa jiji katika maeneo mbalimbali ya kihistoria jijini Dar es salaam.
Wadau wa utalii wakiwa katika Makumbusho ya Taifa jijini Dar es salaam wakiangalia na kujifunza kuhusu enzi za utumwaWalimu wakuu wa sekondari kutoka Shule zaidi 20 za Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam pamoja na wadau mbalimbali wakiwa katika Sanamu la Askari lililopo eneo la Posta.
Afisa Elimu Mwandamizi Makumbusho ya Taifa Anamery Bagenyi akizungumza na waandishi wa habari ambao wameambatana nao katika ziara ya utalii wa jiji akieleza dhamira yao kuandaa utalii wa jiji mara kwa mara.
Afisa Elimu wa Makumbusho ya Taifa kijiji cha Makumbusho Wilhelmina Joseph akiwaeleza wadau wa utalii kuhusu tamaduni zilizopo katika kijiji cha Makumbusho
Mkuu wa Shule ya Charambe ambaye ni Mwenyekiti wa wakuu wa shule TEMEKE Shukuru Nkokelo akizungumzia kuhusu utalii walioufanya siku ya leo.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa utalii.
…………………………
NA MUSSA KHALID
Ili kuendelea kukuza na kutangaza urithi wa Nchi,Makumbusho ya Taifa imewakutanisha takriban Walimu wakuu wa sekondari kutoka Shule zaidi 20 za Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam na wadau mbalimbali kufanya Utalii wa jiji ili kujionea na kujifunza maeneo ya kihistoria.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Leo jijini Dar es salaam ,Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga amesema wamefanya Utalii wa Jiji katika kipindi cha msimu wa Sabasaba ili kuwatembeza wananchi kufahamu historia na urithi wa Nchi yao walikotoka walipo na wanapokwenda.
Aidha Dkt Lwoga amesema kuwa lengo lao ni kutoa elimu kwa wananchi waweze kutambua kuwa fursa za utalii sio mpaka kwenda mbugani badala yake wanaweza kufanya utalii katika miji yao kwani fursa hizo zinasaidia kukuza uchumi wa Nchi.
“Hata katika miji yetu mikubwa ya kitalii zipo fursa nyingi za utalii kama ambavyo zimeonyeshwa katika filamu ya Royal Tour ya Mhe Rais kama Jiji la Dar es salaam kuna eneo la kale ya Magofu ya kale Kunduchi,majumba ya kihistoria na maeneo mengine ambayo ni tunu kwa Taifa”amesema Dkt Lwoga
Dkt Lwoga amesema kuwa ziara kama hizo za utalii mbali na kuendeleza Royal Tour pia ina faida kiuchumi,kijamii na shughuli mbalimbali za uhifadhi.
Afisa Elimu Mwandamizi Makumbusho ya Taifa Anamery Bagenyi amesema lengo lao ni kuhakikisha watanzania wanapata elimu ya kutambua vivutio vilivyopo katika Jiji la Dar es salaam sambamba na kutalii maeneo ya burudani zikiwemo fukwe.
Akizungumzia kuhusu mila,desturi na tamaduni za makabila ya Kitanzania katika kijiji cha Makumbusho Afisa Elimu wa Makumbusho ya Taifa Wilhelmina Joseph ameeleza aina tatu za nyumba zinazopatikana katika kijiji hicho kuwa ni pamoja na Nyumba za msonge,banda na tembe ambazo kwa juu zimekaa tambarare.
‘Kwa mfano nyumba za tembe kwa juu zipo tambarare kwenye paa ambapo unaweza ukakaa juu ya nyumba na kutembela lakini hasa wazee wetu zamani walikuwa wakianika nafaka baada ya kulima mahindi au maboga’amesema Wilhelmina
Kwa upande wao baadhi ya walimu wakuu walioshiriki katika kufanya utalii huo akiwemo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Charambe ambaye ni Mwenyekiti wa wakuu wa shule TEMEKE Shukuru Nkokelo amesema wamejifunza kuhusu Utalii na pia watakuwa mabalozi bora wa utalii kwa kutoa elimu kwa watu kupenda kufanya utalii.
Madam Batuli Ally Mkuu wa Shule ya sekondari Karibuni amewashauri watanzania kujiwekea mazoea ya kufanya Utalii mara kwa mara kwani kufanya hivyo watajifunza na kujionea vivutio mbalimbali ambavyo ni urithi wa nchi.
Hata hivyo amewashauri wahusika wa Makumbusho kuendelea kuonyesha njia kwa wananchi mbalimbali kupenda kujitokeza kufanya utalii na liwe ni jambo endelevu.