……………..
Halimashauri zilizo na maeneo ya vivutio vya utalii kote nchini zimetakiwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau mbalimbali wa Sekta ya Utalii kabla ya kuanzisha tozo mpya kwa watalii wanaotembelea vivutio hivyo ili tozo hizo zisiwe kikwazo kwa Watalii wanaokuja nchini.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana wilayani Wanging’ombe wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya uhifadhi katika Pori la Akiba la Mpanga Kipengere.
Waziri Chana aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Mhe Lauteri Kanoni, ameeleza kuwa jitihada alizofanya na anazoendelea kuzifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan za kuitangaza Sekta ya Utalii kupitia Filamu ya Royal Tour ni lazima ziungwe mkono na wadau mbalimbali na Halimashauri zote kwa kuhakikisha zinaweka mazingira mazuri na rafiki kwa watalii.
Mhe.Waziri Chana ameupongeza uongozi wa Pori la Akiba Mpanga Kipengere kwa kazi kubwa ya usimamizi wa miradi inayotekelezwa akiagiza miradi hiyo ikamilike katika muda uliopangwa kwa ubora na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.