Prof.Philemon Sarungi wakati akikabidhi vitabu 10 maktaba ya Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni vyenye jina la HISTORIA YA UZAWA WA RUMBASI (WATEGI).
Mkurugenzi wa kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Bw. Achilles Bufure akimshukuru Prof. Sarungi kwa kuamua kutoa shukrani ya vitabu kumi ambapo itasaidia Watanzania kufahamu na kujifunza historia ya watu
…………………….
Na Wakirya John
Watanzania wametakiwa kufanya utafiti wa asili yao ili kufahamu historia ya ukoo wao au Taifa lao .
Hayo yamesemwa Leo na Prof.Philemon Sarungi wakati akikabidhi vitabu 10 maktaba ya Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni vyenye jina la HISTORIA YA UZAWA WA RUMBASI (WATEGI) kwa lengo la kutoa shukrani kwa Taasisi hiyo kwa ushirikiano alioupata wakati wa uandaaji wa kitabu hicho.
Prof. Sarungi amesema hana ukabila wala ubaguzi dhumuni la kuandika kitabu hicho cha historia ya Uzawa wa Rumbasi(WATEGI )ni kuhamasisha Watanzania ambao bado hawajafanya utafiti wa asili yao waanze kufanya hivyo.
“Mtu yeyote asiyekuwa na historia ya Ukoo wake au Taifa lake ni sawa na mtumwa”
“Wito wangu kwa Watanzania tujifunze na kujivunia historia yetu” amesema Prof. Sarungi.
Prof. Sarungi ambaye amewahi kuwa Waziri wa Elimu na utamaduni mwaka 1993 amesema kuwa watu watakao tembelea Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni watasoma na kupata kufahamu historia ya watu jamii ya WATEGI.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Bw. Achilles Bufure amemshukuru Prof. Sarungi kwa kuamua kutoa shukrani ya vitabu kumi ambapo itasaidia Watanzania kufahamu na kujifunza historia ya watu jamii ya WATEGI ikiwa historia yao ni kutoka Misri.
“Tutaandaa shindano kwa wanafunzi wanaokuja kutembelea kwenye kituo chetu kwa kutumia maswali shule itakayo fanya vizuri itapata nakala ya kitabu kimoja itakayosaidia watoto wengi kukikosama kitabu hicho. ” alisema Bw. Achilles Bufure.
Naye Afisa Elimu Mwandamizi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Bi Anamery Bagenyi amesema kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni kinapokea watu mbalimbali ikiwemo wageni kutoka nje ya Nchi, hivyo kuleta kitabu hiki hapa itasaidia watu kutoka makabila na mataifa mbalimbali kufahamu historia ya watu jamii ya Wategi.
Kwa upande wao Wafamilia ya Prof. Sarungi wameishukuru sana Makumbusho ya Taifa kwa kuwapa ushirikiano uliopelekea kukamilika kwa uandaaji wa kitabu cha HISTORIA YA UZAWA WA RUMBASI (WATEGI).